*UVCCM kumpa mtaji wa biashara aliyemwagiwa tindikali Igunga
Na Janeth Mushi, Moshi
KATIBU Mkuu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa Martine Shigela, amelaani vitendo vya kikatili vinavyofanywa na baadhi ya vijana kwa itikadi za kisiasa. Amesema vijana kama kundi muhimu nchini linalotegemewa zaidi halina budi kuwa na umoja na kuhakikisha siasa haziwagawi kimakundi.
Amesema vitendo vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya vijana wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) katika Uchaguzi mdogo wa kiti cha Ubunge Ingunga, kwa kummwagia tindikali kijana mmoja kada wa CCM hivi karibuni mkoani Tabora si vya kiungwana na vinatakiwa kukemewa.
Kiongozi huyo wa UVCCM ameyasema hayo jana mjini Arusha alipomtembelea kijana Musa Tesha (24) Mkazi wa Igunga ambaye amekuja katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC kupata matibabu baada ya kumwagiwa tindikali na wanaodaiwa wafuasi wa CHADEMA kabla ya uzinduzi wa kampeni za uchaguzi huo kwa Chama Cha Mapinduzi.
“Hili ni jambo la kulaani kwa yeyote mpenda amani, inasikitisha sana
kwa vijana kutumika na vyama vya siasa kuharibu maisha ya wenzao, nawasihi vijana wenzangu tujiepushe na vyama vya siasa vinavyotaka tufanye fujo na badala yake vijana tunatakiwa kushirikiana katika mambo ya msingi ili tuweze kujenga taifa letu na kuweka itikadi
za vyama vyetu pembeni,” alisema
Amesema kufuatia tukio hilo UVCCM taifa itatoa kiasi cha sh. milioni 5 kwa ajili ya kijana huyo ili akimaliza matibabu aweze kuwa na mtaji wa kuanzia biashara.
“Kwa kweli huu ni unyama usiovumilika siasa zisitufikishe mahali
ambapo mtu anaweza kutoa roho ya mwenzake kwa sababu ya siasa, wanasiasa tunatakiwa kushawishiana kwa hoja, hatuwezi tukagombania fito moja wakati sisi wote ni Watanzania na tunajenga nyumba moja,” alisema Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha James Ole Millya, aliyekuwa ameongozana na Katibu huyo
Akisimulia mkasa huo Musa ambaye ni Mkazi wa wilayani Igunga, alidai
kuwa siku ya tukio alikuwa anabandika mabango ya Mgombea wa CCM, ghafla walitokea wafuasi wa CHADEMA na kumkamata wakidai kuwa
wanampeleka polisi.
Aliongeza Septemba 6, 2011, vijana hao ambao ni wakazi wa Igunga Mjini, baada ya kumchukua badala ya kumpeleka polisi walimpeleka kichakani na kummwagia tindikali usoni na katika mkono wake wa kulia.
“Kwa sasa namshukuru Mungu kwani naendelea vema tofauti na
nilivyoletwa awali toka Igunga, na madaktari wameniambia nisikae mbali na hospitali na baada ya miezi sita nirudi tena kwa ajili ya
kuendelea na matibabu,” alisema Musa
Naye Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Arusha kupitia UVCCM, Catherine
Magige mbali na kuahidi kumchangia kijana huyo sh. milioni moja baada ya matibabu, ameshauri hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya wahusika wa tendo hilo ili iwe fundisho kwa wengine.