Chelsea kushtakiwa na FA

Meneja Andre Villas-Boas akiongea na waandishi wa habari

CHAMA CHA SOKA cha England (FA) kimeishtaki Chelsea kwa kushindwa kuwadhibiti wachezaji wake katika mchezo dhidi ya QPR na kumtaka meneja Andre Villas-Boas kutoa ufafanuzi kuhusu matamshi aliyotoa dhidi ya mwamuzi Chris Foy.
Villas-Boas alisema mwamuzi Foy aliyechezesha mpambano huo alikuwa na maamuzi “duni sana” ambayo yalisababisha timu yake kufungwa 1-0. Wachezaji wawili wa Chelsea walipewa kadi nyekundu na wengine saba kuoneshwa kadi za manjano siku ya Jumapili.
FA itaamua siku ya Jumatano iwapo wamshtaki kwa uwajibikaji mbaya.
Villas-Boas anakabiliwa na adhabu ya faini au kuzuiwa kusimama uwanjani iwapo atakutwa na hatia.
Foy alitoa penati kwa QPR na kuwapa kadi nyekundu Jose Bosingwa na Didier Drogba kabla ya mapumziko. Chelsea imethibitisha kuwa haita kata rufaa dhidi ya kadi hizo.
Alipoulizwa siku ya Jumanne na waandishi wa habari kuhusiana na matamshi yake, Villas-Boas alisema: “Hapana, kwangu mimi kila kitu kiko wazi, kulikuwa na makosa yaliyofanyika.”

BBC