Kanali Gaddafi mwanae wazikwa kisiri Libya

Mwili wa Gaddafi na mfuasi wake ukiwa mjini Misrata

MAZISHI ya Kanali Muammar Gaddafi, mwanae Mutassim na Waziri wa Ulinzi yamefanyika katika sehemu ya siri leo alfajiri. Taarifa zilizotolewa na mmoja wa wasemaji wa Baraza la Kitaifa la Mpito (NTC) ameiambia BBC kuwa miili ya watu hao watatu imezikwa baada ya utata kuhusu kuvutana wapi wazikwe.

Awali baadhi ya ndugu na jamaa wa kabila moja na Kanali Gaddafi waliomba wapewe mwili wa kiongozi huyo ili wauzike mjini Sirte, alipozaliwa lakini inasemekana viongozi wa Baraza la Kitaifa la Mpito walipinga ombi hilo.

Taarifa zingine zinamnukuu msemaji wa NTC Ibrahim Beitalmal akisema jamaa wachache wa familia ya Gaddafi walishiriki katika mazishi hayo na dua zilisomwa kulingana na utaratibu wa Kiislamu.

Baadhi ya watu mjini Misrata wanasema miili ya watu hao watatu iliondolewa usiku kutoka sehemu ilipohifadhiwa katika harakati za kupanga mazishi hayo. Raia wa Libya wamekuwa wakitembelea eneo hilo la Misrata kujionea mwili wa kiongozi huyo ili kuthibitisha ukweli kuwa ameuawa.

Viongozi wa NTC walikuwa wanahofia kuwa huenda Kanali Gaddafi akizikwa katika sehemu iliyowazi, kaburi lake huenda likabadilishwa kuwa pahali patakatifu na wafuasi wake.

Pamoja na hilo mashirika ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakishinikiza uchunguzi ufanyike kubainisha jinsi alivyouawa kanali Gaddafi, kwani picha za awali zilionyesha kuwa alikamatwa akiwa hai.

Kiongozi wa NTC Mustafa Abdul Jalil, ametangaza kuwa uchunguzi utafanyika kuhusu hilo. Hata hivyo, kuna wale wanaohoji ikiwa kweli uchunguzi huo utakuwa wa wazi ikiwa mashirika ya kujitegemea hayata husishwa.
-BBC