TFF yamuengua Michael Wambura kungombea uongozi FAM

Michael Wambura

Na Joachim Mushi

KAMATI ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limemuengu Michael Wambura kugombea nafasi ya uenyekiti katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu mkoani Mara (FAM).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Deogratius Lyatto imesema imeliondoa jina la Wambura kwa kile kukosa sifa ya kugombea nafasi hiyo.

Katika ufafanuzi wake Lyatto amesema mgombea huyo (Wambura) alizivunja katiba ya Klabu ya Simba Ibara 11 (2) (b), Katiba FAM Ibara 12 (2) (e), Katiba ya TFF Ibara 12 (1) (d) na 12 (2) (e), na Katiba ya FIFA Ibara ya 64 (2) mwaka 2010 pale alipompeleka Mwenyekiti wa Simba mahakamani kinyume na Katiba za vyama vyote hapo juu.

Hata hivyo kwa mujibu wa Katiba ya TFF Ibara ya 49 (1), Katiba ya FAM Ibara ya 47, na Kanuni za Uchaguzi za Mwanachama wa TFF Ibara ya 26 (2), Kamati ya Uchaguzi ya TFF kwa kutumia mamlaka yake kikatiba na kanuni za uchaguzi ilimuhoji Wambura juu ya taarifa za kufungua kesi namba 100 mwaka 2010, kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi ya Kisutu, Dar es Salaam.

Amesema Klabu ya Simba mwaka jana katika kikao chake cha Mai 5, 2010 ilimsimamisha uanachama Wambura kwa kukiuka katiba za klabu hiyo kwa kitendo cha kwenda mahakama ya kawaida ya sheria kinyume na taratibu za michezo.

“Kwa kuwa Ndg. Wambura alivunja katiba ya uanachama wa TFF, kwa matakwa ya Katiba hizo hastahili kugombea uongozi wa wanachama wa TFF. Kwa sababu hiyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF inaliondoa jina lake katika wagombea wa FAM,” amesema Lyatto katika taarifa yake. Ameongeza kuwa uchaguzi wa FAM utafanyika Novemba 13, 2011 kama ulivyopangwa.

Hata hivyo Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiomba Sekretarieti ya TFF kumchukulia hatua za kisheria zinazofaa, Wambura dhidi ya kauli za kebei ambazo amekuwa akizitoa kwenye vyombo vya habari kwa kuziita kamati za TFF ‘kangaroo coart’.