Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu nchini (TFF) limetaja wamuzi watakao kuwa na kibarua cha kuchezesha mechi namba 78 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu za Yanga na Simba itakayofanyika Oktoba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Katika taarifa ya TFF iliyotolewa na Ofisa Habari wake leo, Boniface Wambura imemtaja mwamuzi wa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Oden Mbaga kutoka Dar es Salaam kuwa ndiye atakayechezesha pambano hilo.
Wambura amesema waamuzi wasaidizi katika mechi hiyo ambao wote wanatambuliwa na FIFA ni pamoja na Hamis Chang’walu wa Dar es Salaam ambaye atakuwa namba moja, na John Kanyenye (Mbeya) atakayekuwa namba mbili.
“Mtathimini wa waamuzi (referee assessor) atakuwa Soud Abdi kutoka Arusha wakati kamishna wa mchezo huo ni Mohamed Nyange kutoka Dodoma,” amesema wambura katika taarifa yake.
Akitaja viingilio vya pambano hilo litakalofanyika Oktoba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom vitakuwa kama ifuatavyo; Wambura amesema;
“Viti vya kijani na bluu kiingilio kitakuwa sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa ni sh. 7,000, VIP C sh. 10,000, VIP B ni sh. 15,000 wakati VIP A itakuwa sh. 20,000.
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limepanga kuuza tiketi hizo siku moja kabla ya mchezo na siku yenyewe ya mechi katika maeneo ambayo yatatangazwa baadaye,” alisema.