Na Mwandishi Wetu
MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, John Mnyika (Chadema), amesema kuwa atapeleka muswada binafsi wa Sheria ya Udhibiti wa Bei ya bidhaa nchini katika Mkutano ujao wa Bunge unaotarajiwa kuanza Novemba, mwaka huu kutokana na malalamiko ya wananchi kuhusu kasi kubwa ya mfumuko wa bei ya bidhaa.
Mnyika alisema asilimia 70 ya wananchi wanalalamikia mfumuko wa bei ya bidhaa, hali ambayo alisema ni tishio kwa uchumi wa nchi na usalama wa wananchi. Mnyika alisema ikiwepo sheria ya udhibiti wa bei, itasaidia sana kwa kuwa kauli za kisiasa zimeshindwa kudhibiti mfumuko wa bei.
“Napeleka muswada binafsi wa sheria ya udhibiti wa bei ya bidhaa ili tusiishi katika kauli za kisiasa, ambazo zinaongelewa tu bila utekelezaji kwani tangu Waziri Mkuu alipotoa tamko kuwa bei ya sukari ipungue, hakuna utekelezaji,” alisema Mnyika jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Aidha alisema Kauli za Serikali bungeni zilikuwa ni kama danganya toto na kwamba hali inazidi kuwa mbaya hivyo bunge linatakiwa lichukulie kwamba hili ni jambo la dharura na kulifanyia kazi haraka kwa kuweka kifungu kinachotambulisha bidhaa muhimu ambazo bei yake itakuwa inatambulika.
Alisema bidhaa ambazo zitaainishwa kuwa ni muhimu sheria hiyo itapaswa idhibiti bei zake zisipandishwe holela. Mnyika ambaye ni Waziri Kivuli wa Nishati na Madini, aliongeza kuwa athari za mgawo wa umeme zinatokana na mfumuko wa bei hivyo suala hilo linatakiwa litazamwe kama tatizo la sivyo nchi itaingia kwenye machafuko kama ilivyotokea katika nchi nyingine.
Akizungumzia kushuka kwa thamani ya Shilingi ya Tanzania, Mnyika alisema kuwa wananchi hawatakiwi kumwamini Waziri wa Fedha, Mustapha Mkulo, peke yake bali Tume ya Mipango ifuatilie suala hilo na serikali iingilie kati.
“Hatutakiwi kumuamini Mkulo peke yake kwani alishasema sarafu ya Tanzania haitashuka na baadaye ikashuka, nchi yetu inaelekea pabaya,” alisema Mnyika.
Mnyika alimtaka Rais Jakaya Kikwete na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, waingilie kati suala la kuporomoka kwa Shilingi na kusisitiza kwamba hali hiyo ni tishio nchini.
“Hili tatizo sio la Kamati ya Fedha peke yake ni la kamati zopte kwa hiyo kamati zinazoanza vikao leo ziangalie sula hili kwa umakini,” alisema Mnyika.
Aliongeza kuwa katika suala la kupanda kwa bei ya mafuta kila kukicha Mamlaka ya udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) haitaweza yenyewe. “Ufisadi, uzembe na udhaifu ndivyo vinavyotufanya hadi sasa tunanunua gesi nje ya nchi,” aliongeza.
CHANZO: NIPASHE