Jaji akwamisha kesi ya Lema kusikilizwa

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless Lema (CHADEMA)

Na Mwandishi Wetu, Arusha

KESI ya kupinga matokeo ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Godbless
Lema (CHADEMA) leo imekwama kusikilizwa tena baada ya Jaji
anayesikiliza shauri hilo, Aloyce Mujulizi kupata dharura na
kuahirishwa kesi hiyo hadi Oktoba 27, 2011.

Kwa mujibu wa Msajili wa Wilaya Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, George Heberta ambaye alitoa taarifa ya dharura yaani safari ailiyoipata Jaji huyo na kuagiza pande zote kufika mahakamani siku iliyotajwa kuendelea na shauri hilo.

Aidha shauri hilo lililofunguliwa na limefunguliwa na wapiga kura watatu Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo ambao kwa pamoja wanaiomba mahakama hiyo kutengua ushindi wa Lema kwa madai ya kukiuka sheria wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.

Kupitia kwa mawakili wao, Alute Mughwai na Modest Akida, walalamikaji
hao wanadai kuwa katika mikutano ya kampeni, Lema alitoa maneno
kashfa, maneno yaliyolenga ubaguzi wa jinsia na dini kwa aliyekuwa
mgombea kupitia Chama Cha Mapinduzi, Dk. Batilda Burian.

Lema aliyeibuka na ushindi kwa kupata kura 56,196 dhidi ya 37,460
alizopata Dk. Burian anadaiwa kusema kuwa mgombea huyo wa CCM angerejea Zanzibar alikoolewa baada ya uchaguzi huo.

Aidha madai hayo yalipingwa vikali na mawakili wa utetezi, Method
Kimomogolo anayemwakilisha Lema na Timon Vitalis anayemwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao waliieleza mahakaam hiyo kuwa madai hayo yalitakiwa kuwasilishwa mahakamani hapo na Dk. Burian na siyo wapiga kura hao kwa madai kuwa hakuna madhara yoyote waliyoyapata wapiga kura hao.