Watu 13 wajeruhiwa shambulio mjini Nairobi

moja ya majeruhi wa bomu la mkono huko Nairibi Kenya

SHAMBULIO la guruneti katika Mji Mkuu wa Kenya, Nairobi, limesababisha watu 13 kujeruhiwa huku mmoja kati yao kujeruhiwa vibaya kufuatia shambulio hilo.

Taarifa za awali zinasema guruneti hilo limerushwa na mtu asiyejulikana. Taarifa zinaeleza kuwa mtu huyo alifika kwenye eneo la burudani na baada ya mlango kufunguliwa alirusha guruneti na kukimbia.

”Mwanamume mmoja aligonga mlango akijifanya kama mteja na aliporuhusiwa kuingia ndani, akarusha guruneti,” alisema Mkuu wa Polisi mjini Nairobi, Anthony Kibuchi.

Aidha amesema wengi wa waliojeruhiwa walikuwa na majeraha katika sehemu za mikono na miguu. Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumatatu. Majeruhi walikimbizwa katika Hospitali Kuu ya Taifa ya Kenyatta.

Shambulio hili linatokea wiki moja baada ya vikosi vya Kenya kuingia nchini Somalia kukabiliana na wapiganaji wa al-Shabab, ambao Kenya inawashutumu kwa mashambulio na utekaji nyara wa watalii. Al-Shabab walitishia kufanya mashambulio kutokana na hatua hiyo ya Kenya.

-BBC