Arusha yang’ara ‘Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge 2011’

Mshindi wa kwanza wa mbio ndefu za za baiskeli za 'Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge' za kilometa 196, Richard Laizer (Arusha) akimaliza mbio hizo alipotumia saa 5:02:28 katika mbio hizo, zilizoanzia Shinyanga na kumalizikia jijini Mwanza, Mbio hizo ziliandaliwa na Vodacom Tanzania na kudhaminiwa na kinywaji cha Malta Guinness.

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

MKOA wa Arusha jana umeng’ara kwenye mashindano ya mbio za wazi za baiskeli za Vodacom Mwanza (Open Cycle Challenge-2011) baada ya Richard Laizer wa mkoa huo kuibuka mshindi na kuwashinda washiriki zaidi 400 walijitokeza kushiriki kwenye mashindano hayo kwa upande wa wanaume.

Kwa ushindi huo Laizer amejinyakulia sh. milioni 1,500,000 na kuvikwa taji lililokuwa likishikiliwa na Hamis Clement wa Mkoa wa Shinyanga baada ya kutumia muda wa saa 5:02:28 kumaliza mbio za kilometa 196.

Kwa mujibu wa taarifa hizo mshindi wa pili kwa wanaume ni Mindi Mwagi kutoka mkoani Shinyanga aliyetumia saa 5:02:29 ambaye amezawadiwa sh. milioni 1,000,000 akifutiwa na mshindi wa tatu Said Jumanne aliyezawadiwa sh. 700,000 akiwakilisha Mkoa wa Arusha.

Kwa upande wa wanawake, Mkoa wa Arusha uliibuka kidedea baada ya mshiriki wake, Sophia Hussein kuwabwaga washiriki wenzake zaidi ya 60 na kushika nafasi ya kwanza katika mashindano hayo ya kilometa 80 baada ya kutumia saa 2:25:13 kumaliza mbio hizo.

Bi. Hussein amejishindia kitita cha sh. 1,100,000 na kushikilia taji hilo lililokuwa likishikiliwa na Sophia Adison wa Arusha, huku akifuatiwa na mshindi wa pili Bi Mwajuma Musa kutoka mkoani Arusha aliyetumia Masaa 2:25:40 na kujinyakulia zawadi ya shilingi Laki nane.

Hata hivyo mkoa wa Shinyanga nao haukuwa nyuma katika mashindano hayo baada ya Bi Salome Donard baada ya kushika nafasi ya tatu ambapo alizawadiwa kiasi cha sh. 600,000 baada ya kutumia saa 2:26:21 kuhitimisha mbio hizo za kilometa 80 kwa wanawake.

Akizungumza baada ya mashindano hayo, Richard Laizer alisema kilichomsadia ni mazoezi na maandalizi ya mara kwa mara aliyokuwa akiyafanya ingawa mlima wa Bugando wa kumalizia mbio hizo ulimsumbua katika mashindano hayo.

“Nashukuru kwa kumaliza salama na kuwa bingwa katika michuano hii, kutokana na zawadi hii niliyopata kutoka Vodacom Tanzania na wadhamini Wenza Serengeti Breweries kupitia kinywaji chake kisicho na kilevi cha Malta Guinness nitajiendeleza zaidi ili kufikia viwango vya uendeshaji baiskeli kimataifa,” alisema Laizer.

Kwa upande wake Bi. Sophia Hussein alisema mashindano ya mwaka huu kwake yalikuwa na upinzani mkali kwa sababu ushindani ulikuwa ni wa hali ya juu hasa wenye baiskeli za Phoenix ambao walikuwa hawampi nafasi.

Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Kanda ya Ziwa, Steven Kingu, ambae ndiye alikuwa mgeni rasmi aliwapongeza washiriki wote hususani washindi na kuahidi kwamba kampuni yake itaendelea kuratibu, kuandaa michuano hiyo ili kuifanya kufikia michuano ya kimataifa.

“Nimefarijika kwa mbio hizi za wazi za Vodacom Mwanza Open Cycle Challenge kuendelea kuwa bora kila mwaka na hili linatupa changamoto za kuendelea kuandaa na kudhamini katika mikoa mingine kama sio Tanzania nzima,” alisema Kingu.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Serengeti Breweries Limited (SBL) Ephraim Mafuru ambao ni wadhamini wenza kupitia kinywaji kisicho na kilevi cha Malta Guinness alisema hawajutii kudhamini michuano hiyo kutokana na hadhi iliyonayo.

“Tumeshuhudia kupitia udhamini wetu washindi wamejipatia zawadi ambazo kama watazitumia vema zinaweza kuwa mitaji itakayowawezesha kujiletea maendeleo katika ngazi ya familia na Taifa kwa ujumla,” alisema Mafuru.