Maiti ya Gaddafi yakaguliwa Mjini Misrata

Mwili wa Kanali Gaddafi ukiwa umelazwa chini baada ya kufariki dunia.

OFISA anayechunguza vifo vya ghafla nchini Libya anakagua mwili wa Kanali Muammar Gaddafi leo, huku bado idadi kubwa ya watu ulimwenguni wakihoji namna kiongozi huyo alivyo uwawa.

Taarifa kutoka nchini Libya zinaeleza kwa sasa maiti ya Gaddafi iko katika chumba cha barafu (jokofu) cha kuweka nyama mjini Misrata – ikiwa na alama ya risasi kichwani.

Familia ya Kanali Gaddafi inataka maiti yake itolewe. Lakini haijulikani atazikwa wapi. Maofisa wa juu wa Serikali ya Mpito wamesema sherehe rasmi itafanywa kesho, kutangaza kuwa Libya imeshakombolewa.

Marekani na Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa Libya kufanya uchunguzi wa wazi juu ya kifo cha Kanali Gaddafi. Kuna shaka kuwa aliuliwa kusudi, siyo kwa ajali, katika mapambano ya risasi, kama ilivoelezwa rasmi na wakuu wa Libya.

Maiti ya Gadaffi imewekwa katika chumba cha barafu (jokofu) cha kuweka nyama mjini Misrata. Ofisa mhusika anatarajiwa kukagua maiti hiyo kikamilifu hii leo. Wananchi wa Libya wanapiga foleni kwenda kuona maiti ya kiongozi huyo wa zamani pamoja na mtoto wake, Mo’tassim, ambaye piya aliuwawa Alkhamisi.

Kila mtu anazungumza juu ya video iliyopigwa kwenye simu ya mkononi, inayoonesha dakika za mwisho za kiongozi huyo, kabla ya kufa.

Viongozi wa serikali ya muda ya Libya lazima waamue kama watamzika hadharani au watafanya maziko ya siri na haraka, kabla ya kutangaza ukombozi kamili wa Libya hapo kesho, na kutoa tarehe ya uchaguzi wa kidemokrasi.