Ndege yaanguka Arusha yaua na kujeruhi

Ndege iliyoanguka

Na Mwandishi Wetu, Arusha

NDEGE ndogo ikiwa na marubani wawili imeanguka na kusababisha kifo cha mmoja wao huku mwingine akijeruhiwa vibaya. Rubani aliyepoteza maisha katika ajali hiyo ni Ally Harun (24) na mwenzake, Liliani Koima akijeruhiwa vibaya na kulazwa hospitali ya rufaa ya KCMC, mkoani Kilimanjaro Moshi.

Ndege hiyo yenye usajili namba 5H/QTE mali ya kampuni ya World
Quality Travel & Tours ya jijini Arusha ilianguka wakati ikielekea
kutua kwenye uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) baada
ya kushindwa kutua kwenye uwanja mdogo wa ndege wa Arusha kutokana na kukosekana kwa taa kwenye njia ya kutua na kuruka uwanjani hapo.

Akizungumzia tukio hilo leo mjini hapa, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa amethibitika kutokea kwa ajali hiyo kwenye Kijiji cha Samaria wilayani Arumeru, juzi Alhamisi majira ya Saa 1:55 usiku walipokuwa wakisubiri ruhusa ya kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Alisema kuwa rubani Kolina anaendelea kupatiwa matibabu kwenye kwenye hospitali ya KCMC ambako hali yake inadaiwa kuendelea kuimarika huku mwili wa Haruna ukiwa umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya mkoa wa Arusha ya Mount Meru.

Akielezea tukio hilo, Mpwapwa amesema ndege hiyo ilitokea jijini Dar es Salaam ilifika katika uwanja mdogo wa Arusha lakini akashindwa kutokana na uwanja huo kukosa huduma ya taa kwa sababu ambazo hazijajulikana hadi sasa iwapo ni mgawo wa umeme au hitilafu ya kiufundi.

Alisema kuwa marubani hao walielekezwa kwenda kutua KIA ambapo
walifanya mawasiliano na waongoza ndege wa uwanja huo na kuwaruhusu baadaye walipoteza mawasiliano na ndipo ikapatikana taarifa za ajali hiyo.

Mpwapwa alisema kuwa ndege hiyo ilianguka jirani na nyumba ya Maria
Akyoo ambapo mbuzi wake watatu walikufa na banda lake lililokuwa
pembeni ya nyumba hiyo kuharibiwa kabisa.

Taarifa zilizopatikana kwa walioshuhudia ajali hiyo zinaeleza kuwa
kabla ya kuanguka, ndege hiyo ilionekana ikizungukazunguka kwa muda
mrefu maeneo ya karibu na kijiji hicho katika kile kinachodaiwa
kusubiri maelekezo ya kuruhusiwa kutua.

Sababu za kukosekana kwa taa uwanjani hapo zilishindikana baada kila
mfanyakazi aliyeulizwa kutokuwa tayari kutoa ushirikiano kwa waandishi
wa habari huku wakikataa kusema alipo meneja wa uwanja.

Hata baada ya kupatikana kwa njia ya simu yake ya kiganjani, meneja wa uwanja huo, Simon Kimiti alikataa kuzungumzia ajali hiyo na kuelekeza atafutwe mwenzake wa KIA aliyedai ndiye mhusika.