TANZNIA imepongezwa kwa jitihada zake za kutekeleza Malengo ya Milenia ambayo yalilenga katika kupunguza vifo vya akina mama na watoto na pia jitihada zake katika kupambana na ugonjwa wa Ukimwi na athari zake.
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN) Dkt. Asha Rose Migiro ameyasema hayo leo asubuhi Ikulu ambapo amekuja kuleta ujumbe maalum kwa Rais kutoka kwa Katibu Mkuu wa UN Bw. Ban Ki Moon.
“Katibu Mkuu anakuomba uendelee na juhudi zako hizo wakati tunaelekea mwaka 2015 ambapo UN iliweka malengo ya kupunguza vifo vya akina Mama na Watoto na pia kupunguza Maambuziki ya Ukimwi” Naibu Katibu Mkuu amesema.
Mama Migiro amesema hivi sasa UN inawahamasisha wanachama wake waanze kufikiria kitu gani kifanyike baada ya mwaka 2015 na kuziomba nchi zitoe maoni na mapendekezo ya jinsi mafanikio yaliyokwisha fikiwa hadi sasa yanaweza vipi kudumishwa na kuendelezwa zaidi ili hatimaye matatizo hayo yaliyoko kwenye malengo ya milenia yaweze kupunguzwa na ikiwezekana kuondoshwa kabisa.
Mama Migiro amesema UN inatambua kuwa malengo ya milenia yanaweza kusaidia katika kuchochea maendeleo na hivyo ni vyema yakadumishwa na kuendelezwa zaidi ili jitihada za kupunguza umaskini ziweze kufanikiwa.
Mama Migiro amemueleza Rais Kikwete kuwa UN inatambua jitihada za Rais Kikwete za kupambana na Ukimwi na Malaria, jitihada ambazo zinahesabiwa na UN kuwa zimeleta matumaini na manufaa makubwa katika nchi mbalimbali duniani.
Rais Kikwete amekuwa mshiriki mkubwa katika malengo ya Milenia kwa kujihusisha na kuweka juhudi kubwa katika kupunguza vifo vya akina Mama na Watoto, jitihada katika kupambana na malaria na sekta ya afya kwa ujumla.
Rais Kikwete amekuwa mshiriki mkuu katika kamati mbalimbali za kimataifa zikiwemo African Leaders Malaria Alliance (ALMA) ambapo jitihada hizi zimefanikisha kuongeza matumizi ya vyandarua, dawa za kunyunyizia kwa ajili ya kuua vimelea vya malaria na matumizi ya dawa mseto ambayo imekuwa na nguvu zaidi katika kuua malaria tofauti na dawa ambazo zilikuwa sugu hivyo kutokuwa na nguvu za kutibu malaria hapa nchini.
Rais Kikwete pia amekuwa Mwenyekiti Mwenza kwenye kamati ya Katibu Mkuu wa UN, juu ya Afya ya Mama na Mtoto ambayo imekuwa ikifuatilia na kutizama uwekaji na upatikanaji wa taarifa sahihi kuhusu Afya ya Mama na Mtoto ili kufanikisha katika kutoa huduma bora za Uzazi Salama, Kamati hiyo inajulikana kama, Commission on Information and Accountability for Women’s and Children’s Health.
Mapema zaidi Rais amekuwa Mwenyekiti Mwenza katika jitihada za Helsink (Helsink Process on Global and Democracy) jitihada ambazo zinalenga katika kutoa jukwaa la majadiliano na maafikiano baina ya serikali, mashirika ya kijamii na kibiashara.
Katika kikao cha mwisho cha UN mwezi Septemba mwaka huu, Rais Kikwete amepokea tuzo mbalimbali za UN kama ishara ya kutambua juhudi hizo za Tanzania na Rais wake kwa ujumla. Tuzo hizo ambazo ni Tuzo Maalum Juu ya Afya na Teknolojia; Tuzo ya Afya ya Mama Mjamzito na Watoto na Tuzo ya kutoka Soko la Hisa la Marekani (National Association of Securities Dealers Automated Quotations – NASDAQ)