WAMA, GE kushirikiana kupunguza vifo vya wajawazito na watoto

Mwenyekiti wa Taasisi, Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo

TAASISI ya General Election Health Magination (GE) ya nchini Marekani imeamua kufanya kazi na Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ili kuhakikisha kuwa vifo vya wanawake wajawazito na watoto vinapungua hapa nchini.

Hayo yamesemwa jana na Mkurugenzi wa Programu wa Taasisi hiyo Janeen Uzzell wakati akiongea na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete alipomtembelea ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam.

Uzzel alisema kuwa wameamua kufanya kazi na Taasisi ya WAMA kutokana na jitihada zinazofanywa na Mwenyekiti wa Taasisi hiyo Mama Salma Kikwete za kuhakikisha kuwa vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua kwa kuchangia vifaa tiba katika Hospitali, vituo vya Afya na Zahanati na kutoa elimu ya uzazi salama kwa jamii.

“Katika suala la kupunguza vifo vya kina mama wajawazito na watoto Taasisi yetu inafanya kazi tatu ambazo ni kufuatilia maendeleo ya Mama mjamzito tangu mimba iko changa hadi wakati wa kujifungua, tunatoa mashine ya kumsaidia mtoto mchanga na mama mjamzito pale ambapo mama atakuwa amejifungua na hana nguvu za kumsaidia mtoto na vifaa tiba vya kuwahudumia wagonjwa wa dharula,” alisema Uzzell.

Kwa upande wake Mama Kikwete aliishukuru taasisi hiyo kwa kuona umuhimu wa kuimarisha afya ya mama na mtoto na hivyo kuamua kufanya kazi nchini Tanzania kwa ajili ya kukabiliana na tatizo hilo.

Alisema kuwa Afrika inahitaji kusaidiwa ili iweze kuimarisha afya ya mama na mtoto kwani vifo vya mama na mtoto ni tatizo katika nchi nyingi za Afrika ikiwemo Tanzania ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali inafanya kila liwezalo ili kuhakikisha kuwa malengo ya milinia namba nne na tano yanafanikiwa ifikapo mwaka 2015.