SALOMON Kalou, mchezaji wa Ivory Coast ambaye huichezea Chelsea, ameielezea klabu hiyo kupata hakikisho kwamba atacheza mechi zaidi, kabla ya kukubali kutia saini mkataba mpya Stamford Bridge.
Kalou, mwenye umri wa miaka 26, ameamua kuondoka katika klabu hiyo mara mkataba wake utakapokwisha msimu huu, kwani anakerwa kwa kutocheza mechi kila wikendi
Naye Meneja Andre Villas-Boas alifichua wiki iliyopita kwamba majadiliano yameanza ikiwa ataweza kumuongezea Kalou mkataba kucheza msimu ujao.
Pande zote mbili lazima kufikia makubaliano kabla ya mwezi Januari, ikiwa Chelsea itaweza kuepuka hatari ya Kalou kuondoka pasipo klabu kupata senti zozote.
Salomon Kalou amecheza katika mechi mbili tu za Chelsea msimu huu, kati ya mechi 12, na moja kati ya mechi hizo ikiwa ni ya Kombe la Carling.
Kalou alifanikiwa kufunga bao, alipoingia katika nusu ya pili ya mchezo Jumatano usiku, wakati Chelsea ilipofanikiwa kuifunga Genk ya Ubelgiji magoli 5-0 katika mechi ya uwanja wa nyumbani wa Stamford Bridge, ikiwa ni mechi ya ligi ya klabu bingwa Ulaya.
Mchezaji huyo ameichezea Chelsea kwa muda wa miaka mitano sasa, amesema angelipenda kushirikishwa zaidi katika mechi.
“Hicho ndicho anachokitaka kila mchezaji, nafasi ya kucheza,” alielezea Kalou.
“Ikiwa haupati nafasi ya kucheza kila mwishoni mwa wiki, ni vipi utaweza kuimarisha kiwango chako cha mchezo?
“Kwa hiyo ni muhimu sana kucheza kadri ya kiwango chako chote. Hilo ndilo ninalolitazamia.”
Licha ya kucheza mara mbili kama mchezaji wa zamu katika mechi ya Kombe la Carling na ya klabu bingwa, Kalou hajapata kucheza hata angalau dakika moja katika mechi ya ligi kuu ya Premier tangu tarehe 20 mwezi Agosti.
-BBC