Ujenzi wa Kituo cha Wanafunzi UDSM ni msaada kwa wanafunzi- JK

Baadhi ya Majengo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM)

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Tanzania Jakaya Kikwete amesema kuwepo kwa Kituo cha Wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kutakidhi mahitaji mengi mbalimbali ya wanafunzi hasa wale wanaokaa nje ya chuo hicho.

Rais Kikwete ametoa kauli hiyo jana Dar es Salaam alipokuwa kwenye harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo hicho cha wanafunzi katika chuo cha UDSM.

Akizungumza kwenye hafla hiyo amesema wanafunzi wanaokaa nje ya chuo wanahitaji mahali pa kujisomea, mahali pa kupumzika wanaposubiri vipindi au mahali pa kuzungumza na wenzao au wageni wao wanapowatembelea huduma ambayo haipo kwa sasa hivyo wanafunzi kuzagaa hovyo.

“Kwa wale wanaoishi nje ya Chuo wanapokuwepo Chuoni kwa masomo, wanahitaji mahali pa kujisomea, mahali pa kupumzika wanaposubiri vipindi au mahali pa kuzungumza na wenzao au wageni wao wanapowatembelea. Hivi sasa wanazagaa zagaa tu chini ya miti au kwenye corridors. Kwa kweli wanapata taabu hasa wakati wa jua kali na mvua,” alisema Kikwete.

Amesema kujengwa kwa kituo hicho kutamaliza adha wanazopata wanafunzi zitapungua hasa kwa wale wanaoishi njie ya Chuo na hata wale wanaoishi Chuoni.
Ameongeza kuwa kuna haja ya kuboresha mazingira ya maisha ya wanafunzi chuoni hasa malazi, yaani mahali pa kuishi, kujisomea, kupumzikia na kujipatia huduma mbalimbali kama vile chakula, burudani na mengineyo.

Rais Kikwete amesema ongezeko kubwa la haraka la udahili katika Chuo Kikuu katika miaka ya hivi karibuni limefanya mahitaji yahusuyo mazingira ya maisha ya wanafunzi kuwa changamoto kubwa.

“Kwa upande wa malazi, chuo hakijaweza kuwapatia wanafunzi wote nafasi ya kulala hapo chuoni hivyo kulazimika kujenga hosteli nje ya Chuo huko Mabibo na kununua hosteli ya NBC Ubungo na nyumba za CRDB Kijitonyama. Hata hivyo, bado wapo wanafunzi wengine ambao wamekosa nafasi hata kwenye hosteli hizo na kulazimika kujitafutia wenyewe malazi ya kupanga,” anasema Kikwete.

Amebainisha kuwa chuo na Serikali wanaendelea kushughulikia suala la kuwapatia wanafunzi malazi mazuri ili wasilazimike kupanga mitaani.

Aidha aliwapongeza viongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa kubuni mradi huu muhimu na hasa kwa uamuzi wa busara wa kuwashirikisha wana-kaya ya Chuo hiki na Watanzania wengineo wakereketwa wa elimu.

“Hii ni mara ya kwanza kwa wahitimu wa Chuo Kikuu chetu kikongwe kuliko vyote nchini kukutana kwa shughuli ya uchangiaji wa maendeleo ya taasisi yao iliyowapatia ufunguo mkubwa wa maisha, elimu ya juu. Aghalabu, tumezoea utaratibu kama huu ukitumika kwa shule za sekondari na hata za msingi. Nafurahi kuona kwamba busara imewaongoza kutumia maarifa hayo ili sisi tulio wahitimu na wafanyakazi wa Chuo hiki tuchangie katika maendeleo yake,” amesema katika hotuba yake.

“Bila ya shaka tunatambua juhudi kubwa zilizofanywa na viongozi wetu waasisi wa taifa, hususan Baba wa Taifa na viongozi wenzake wa Chama cha TANU kabla na baada ya mwaka 1961 na baadae Muungano wa mwaka 1964 za kuendeleza elimu ya juu hapa nchini. Mtakumbuka pia kwamba uamuzi wa busara na wa kishujuaa uliofanywa na Chama cha TANU wa kukabidhi jengo lake ililolijenga kwa nia ya kuwa Makao Makuu yake pale Lumumba ili litumike kuanzisha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Baadaye mwaka 1964 ujenzi ulipokamilika wa majengo katika makao rasmi, ambako kwa sasa panajulikana kama Mlimani, ndipo Chuo kilipohama kutoka mtaa wa Lumumba.”

“Juhudi hizo zimeleta mafanikio makubwa. Chuo Kikuu kilichoanza na Kitivo kimoja cha Sheria chenye wanafunzi 13 leo kinazo takriban fani zote kuu za kitaaluma na wanafunzi wapatao 16,000. Kwa sasa Vyuo Vikuu nchini vimeongezeka na kufikia 35 vyenye wanafunzi 135,367. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kimezaa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine mwaka 1984 na Chuo Kikuu cha Sayansi ya Afya na Tiba cha Muhimbili mwaka 2007. Aidha, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam pia kilikilea kilichokuwa Chuo cha Ardhi hadi kuwa Chuo Kikuu kamili mwaka 2007,”