MAJARIBIO ya chanjo ya malaria barani Afrika yametoa matumaini ya kupatikana kwa chanjo ya kwanza diniani ya ugonjwa huo, unaoenezwa na mbu. Watoto waliopata chanjo hiyo ya majaribio wana nafasi nusu ya kupata ugonjwa huo.
Zaidi ya watoto 15,000 chini ya miezi kumi na minane walihusishwa katika utafiti huo uliochapishwa katika jarida linalojadili maswala ya kimatibabu la New England Journal of Medicine. Majaribio hayo yalifanywa katika nchi saba barani Afrika kwa makundi mawili ya watoto- waliozaliwa hadi wiki 12- na watoto wa miezi mitano hadi miezi 17.
Katika kipindi cha mwaka mmoja, watafiti wamegundua visa vilivyoripotiwa vya malaria vilikuwa vimepungua kwa nusu katika kundi la watoto wakubwa kidogo waliopewa chanjo hiyo, ikilinganishwa na wale waliopata chanjo dhidi ya magonjwa mengine.
Chanjo hiyo yenye jina ‘RTS-comma-S’ ilitengenezwa na kampuni ya GlaxoSmithKline, na ni mojawapo ya chanjo mbili dhidi ya malaria zinazofanyiwa majaribio duniani. Ugonjwa wa malaria huuwa watu 800,000 kila mwaka, wengi wakiwa ni watoto barani Afrika. Takriban watu millioni 225 huambukizwa ugonjwa wa malaria kila mwaka.
-BBC