Taifa Stars kuingia kambini dhidi ya Chad

Baadhi ya wachezaji wa Taifa Stars

Na Mwandishi Wetu

TAIFA Stars inatarajia kuingia kambini Novemba 3 mwaka huu kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayofanyika Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na ofisa Habari wa TFF leo mjini Dar es salaam, Boniface Wambura amesema wachezaji watakaoitwa Stars wanatakiwa kuripoti kambini ndani ya muda uliopangwa, mechi za mwisho kumaliza mzunguko wa kwanza Ligi Kuu ya Vodacom zimefanyiwa marekebisho. Mechi hizo sasa zitachezwa Novemba 2 mwaka huu badala ya tarehe ya awali ya Novemba 5 mwaka huu.

Amesema mechi hizo ni Oljoro vs Villa Squad (Uwanja wa Sheikh Kaluta Amri Abeid), Moro United vs Simba (Uwanja wa Taifa), Polisi Dodoma vs Yanga (Uwanja wa Jamhuri), Toto Africans v Azam (Uwanja wa CCM Kirumba), Kagera Sugar vs Coastal Union (Uwanja wa Kaitaba), Mtibwa Sugar vs African Lyon (Uwanja wa Manungu) na Ruvu Shooting vs JKT Ruvu (Uwanja wa Mlandizi).

Wakati huo huo akizungumzia mechi namba 58 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Kagera Sugar iliyochezwa Oktoba 14 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, Wambura amesema iliingiza sh. 42,810,000. Watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 11,559.

Watazamaji 11,787 walikata tiketi kushuhudia mechi namba 62 ya ligi hiyo kati ya Simba na African Lyon iliyochezwa Oktoba 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Mechi hiyo iliingiza sh. 41,800,000.

Nayo mechi namba 60 kati ya JKT Ruvu na Azam iliyochezwa Oktoba 15 mwaka huu kwenye Uwanja wa Azam Chamazi iliingiza sh. 909,000 kutokana na watazamaji 303 waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo.

LIGI DARAJA LA KWANZA
Ligi Daraja la Kwanza hatua ya makundi inayochezwa kwa mtindo wa nyumbani na ugenini inaendelea tena kesho (Oktoba 19 mwaka huu) kwa mechi saba katika viwanja tofauti.

Katika kundi A, Polisi Dar es Salaam itacheza na Burkina Faso ya Morogoro kwenye Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani wakati Transit Camp itakuwa mwenyeji wa Temeke United kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga. Nayo Mgambo Shooting itakuwa mgeni wa Morani katika mechi itakayochezwa mkoani Manyara.

Kundi B itakuwa kati ya Small Kids na Tanzania Prisons zitakazocheza mjini Morogoro, Mbeya City itaumana na Mlale JKT kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine. Kundi C ni kati ya Manyoni FC na Polisi Morogoro itakayochezwa mjini Singida wakati Rhino FC itakuwa mwenyeji wa AFC kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.

Mechi kati ya Majimaji na Polisi Iringa ya kundi A yenyewe itachezwa Oktoba 20 mwaka huu Uwanja wa Majimaji mjini Songea kama itakavyokuwa kwa mechi ya kundi C kati ya 94KJ na Polisi Tabora itakayochezwa Uwanja wa Mlandizi mkoani Pwani.

Aidha akizungumzia viingilio katika mechi namba 66 kati ya Simba na Ruvu Shooting itakayochezwa Oktoba 19 mwaka huu Uwanja wa Azam Chamazi, Dar es Salaam amesema itakuwa ni sh. 10,000 kwa VIP na sh. 5,000 kwa mzunguko. Tiketi za mechi hiyo zitauzwa uwanjani Chamazi katika magari maalumu kwa ajili ya shughuli hiyo.