Saudi Arabia kuwasilisha malalamiko Baraza la Usalama

Rais wa Iran, Mahmoud Ahmedinejad

UONGOZI wa Saudi Arabia unataka kuyawasilisha katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, malalamiko baada ya kubainika njama ya kumuua balozi wake nchini Marekani. Inadaiwa kuwa Iran ilihusika na upangaji wa njama hiyo. Hata hivyo, kwa mujibu wa balozi wa Saudi Arabia katika Umoja wa Mataifa, inachokitaka serikali yake bado hakijakuwa bayana.
Kwa upande wa, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tayari imeshaiwekea Iran vikwazo kwa awamu nne kwasababu ya mpango wake wa nyuklia unaozua utata. Urusi na China zilizo na uhusiano wa karibu wa kibiashara na Iran, zinaripotiwa kuwa na hisia tofauti kuhusu madai hayo.
Ifahamike kuwa watu wawili tayari wamefikishwa mahakamani mjini NewYork kufuatia tukio hilo lililodhamiria kumuua balozi wa Saudi Arabi nchini Marekani, Adel al- Jubeir. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, alithibitisha kuwa alishaiwasilisha katika Baraza la Usalama la jumuiya hiyo, barua ya ombi la Saudi Arabia pamoja na malalamiko ya Iran na Marekani.
Rais wa Iran, Mahmoud Ahmedinejad ameyakanusha madai hayo ya serikali yake kuhusika na njama hiyo ya mauaji.

-DW