WAFUNGWA wapatao 295 wa Palestina wataachiwa kati ya kundi la 477 waliorodheshwa. Shughuli hiyo inatazamiwa kuendelea kwa muda wa saa kadhaa. Magari ya kwanza ya msafara huo yatakayowasafirisha wafungwa wa kike tayari yameondoka kwenye jela moja yakielekea eneo la Ukingo wa Magharibi. Maofisa wa Usalama wa Misri, iliyousimamia mchakato huo wa kufikia makubaliano ya kubadilishana wafungwa, ndio wanaousindikiza msafara huo.
Misafara ya magari yatakayowasafirisha wafungwa wa Palestina imeanza kuondoka katika magereza ya Israel kama ilivyoafikiwa katika mpango wa kubadilishana wafungwa.
Kulingana na mpango huo, mwanajeshi wa Israel, Gilad Shalit ataachiwa huru na kurejea nyumbani baada ya kuzuiliwa kwenye Ukanda wa Gaza tangu mwezi wa Juni mwaka 2005.
Aviva Shalit, mamake mzazi Gilad Shalit anasisitiza kuwa leo ni siku ngumu ijapokuwa mwanawe anaachiwa huru. Kwa upande wao, viongozi na wafuasi wa kundi la Hamas wanajiandaa kuwapokea wafungwa hao wa Palestina kwa shangwe na nderemo. Palestina wengine 550 wataachiwa huru katika awamu ya pili ya mpango huo wa kubadilishana wafungwa.
Wakati huohuo, washauri wa kimataifa wa kundi la pande nne wanajiandaa kukutana mjini Jerusalem tarehe 26 mwezi huu ikiwa ni katika harakati za kuufufua mchakato mzima wa kuisaka amani ya kudumu ya eneo la Mashariki ya Kati.
-DW