Al-shabab kulipiza kisasi, kuipiga Kenya

Wanamgambo wa Al- shabaab

MSEMAJI wa kundi la wapiganaji wa Al-Shabab, Sheikh Ali Dheere amesema wako tayari kulipiza kisasi kwa kuyashambulia majengo ya Kenya na kuzorotesha uchumi wa nchi hiyo. Akizungumza na Idhaa ya Kisomali ya BBC, Sheikh Dheere amenukuliwa akisema; “Tunaiambia serikali ya Kenya na watu wake kuwa wametangaza vita, hawajui vita ni nini, ni kubomoa majengo ya orofa na yanayopendeza nchini Kenya ambayo yanatambuliwa kwa uzuri wake Afrika na vile vile kuzorotesha utalii”
Sheikh huyo aliongeza kuwa “Kwa miaka mingi tumepigana na serikali zenye nguvu zaidi na kwa nguvu za Mungu tumeweza kukabiliana nazo na kuzishinda na sasa tunaiambia Kenya inapaswa itafakari tena kuhusu hili, nyinyi mmebarikiwa na amani, mtu ambaye anaishi katika jengo la vioo hapaswi kuwavurumishia watu mawe. Huu ndio ujumbe tunataka uifikie Kenya.”
Awali Waziri wa Mashauri ya Nchi za Kigeni wa Kenya Bw. Moses Wetangula aliiambia BBC kuwa nchi yake imepeleka majeshi nchini Somalia kukabiliana na wapiganaji wa al-Shabab. ‘Mashambulizi ya angani’
Bw. Wetangula amesema Kenya inajilinda na hii ni baada ya mfululizo wa utekaji watu nyara unaoshukiwa kutekelezwa na al-Shabab.
Watu walioshuhudia wanasema wameona magari mengi ya kijeshi eneo la mpakani ikiwa nipamoja na ndege na helikopta. Taarifa zasema al-Shabab, ambao wamekanusha kuhusika na utekaji huo wameanza kujiandaa kupigana.
Raia kadhaa kutoka mataifa ya magharibi wametekwa nchini Kenya na watu wanaoshukiwa kuwa wanamgambo wa Kisomali na kupelekwa Somalia. Wiki iliyopita, maafisa wawili wa shirika la kutoa misaada, la madaktari wasio na mipaka (MSF) walitekwa katika kambi ya wakimbizi ya Dadaab, kaskazini ya Kenya.
Wageni wengine wawili pia walitekwa nyara hapo kabla katika mji wa Lamu, mwambao wa Kenya. Wageni hao ni pamoja na watalii wawili, raia mmoja wa Uingereza na mwengine wa Ufaransa.

Mwandishi wa BBC aliye kaskazini mashariki ya Kenya anasema wanajeshi wa Kenya waliingia Somalia Jumapili asubuhi. Kuna taarifa za kutatanisha kuhusu ni nani hasa mtekaji nyara- kuna baadhi ya watu wanadai utekaji huo unatekelezwa na al-Shabab na wengine wanasema ni makundi ya maharamia.
Baada ya miaka 20 ya mzozo Somalia, silaha zimesambaa na ni rahisi kupatikana nchini Somalia na huenda utekaji nyara huu ni kazi ya kundi jingine lenye silaha la Somalia. Bw. Wetangula amesema wanajeshi wamevuka mpaka na kuingia Somalia kwa radhi ya serikali ya mpito ya Somalia ambayo inadhibiti eneo dogo tu.
Mwandishi wa BBC anasema habari alizopata kutoka Somalia zinaarifu kuwa wanajeshi wa Kenya wameingia na vifaru hadi kilomita 90 ndani ya Somalia.

-BBC