Maandamano duniani kote ya kupinga kile waandamanaji wanakiona kama uroho na usimamizi mbaya wa uchumi duniani yameingia siku ya pili.
Katika miji kadhaa – kutoka Auckland hadi Toronto – waandamanaji walikesha katika mahema kushinikiza wanasiasa wachukue hatua.
Haijawa wazi iwapo maandamano yanaanza kushikamana na kuwa kitu kikubwa.
Mjini London, msemaji alisema lengo ni kuiga mambo yanayotokea mjini New York, katika mtaa wa masoko ya fedha, ambako maelfu ya watu wamekuwa wakiandamana kwa wiki kadhaa.
Mjini London waandamanaji wamelala nje ya kanisa kuu la Saint Paul, katikati ya jiji, baada ya kuondoshwa jana nje ya Soko la Hisa.
Watu kama 500 walibaki, na wengi wao walilala kwenye mahema kama 70, wengine walikaa juu ya ngazi nje ya kanisa.
Wana kauli moja – wamekerwa na serikali ya mseto ya Uingereza kubana matumizi, na wamehamaki kuwa mabenki yanasaidiwa.
Biramu moja linasema “mwisho umefika”.
Wanalalamika kuwa demokrasi haifanyi kazi na wanasema watabaki hapo wakiwa ni sehemu ya vuguvugu la dunia.
Baadhi yao wanasema wanaweza kubaki hapo hadi Disemba.
-BBC