Na Mwandishi Wetu, Mpanda
KAMPUNI ya Simu za Mkononi ya Vodacom inashiriki Mkutano wa Uwekezaji katika Ukanda wa Ziwa Tanganyika ulioanza jana mjini Mpanda kwa maonesho ya bidhaa na huduma kutoka wadau anuai wa uwekezaji nchini.
Akitoa maelezo ya huduma na bidhaa za Vodacom kwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliyetembelea banda la Vodacom katika maonesho hayo, Meneja Mawasiliano wa Vodacom, Salum Mwalim amemueleza Pinda kuwa Vodacom inaunga mkono juhudi za Serikali kuinua kiwango cha uwekezaji kwa Ukanda wa Ziwa Tangayika.
Mwalim amemweleza Waziri Mkuu kuwa inaunga mkono juhudi za Serikali za kushawishi uwekezaji katika eneo hilo hatua ambayo itasaidia kuinua uchumi wa mikoa ya Tabora, Kigoma na Rukwa pamoja na ustawi wa jamii za wakazi wa mikoa hiyo.
“Vodacom siku zote tunafurahia maendeleo ya nchi na wananchi na tumekuwa washirika wa maendeleo kwa vitendo, tumekuwa tukifanya juhudi za makusudi katika kubadili maisha ya watanzania kupitia tekenolojia ya simu za mkononi kupitia shabaha yetu ya kuwaunganisha watu, kutengeneza fursa na kubadili maisha,” alisema Mwalim.
Meneja huyo wa Mawasiliano wa Vodacom ameongeza kuwa Vodacom tayari imeshawekeza kwa kiasi kikubwa katika ukanda huo hivyo kutoa uhakika wa mawasiliano wa sauti na data kwa wawekezaji wote watakaojitokeza kama ambavyo wananchi na wadau wengine wanavyofurahia mawasiliano ya mtandao huo wa Vodacom hivi sasa.
“Mh. Waziri Mkuu kama tunavyotambua biashara katika ulimwengu wa sasa unahitaji sana huduma ya uhakika wa mawasiliano hivyo hatua yetu ya kuwekeza katika ukanda huu bila shaka yatasaidia juhudi za serikali za kuhamasisha uwekezaji katika eneo hili”Aliongeza Mwalim na kuungwa mkono na Waziri Mkuu Pinda.
“Ni kweli huduma za mawasiliano ni muhimu sana Vodacom mnafanya vizri wananchi wanapata huduma za simu ukanda huu wa ziwa Tanganyika ila ongezeni juhudi”Alisema Waziri Mkuu Pinda akiwa katika banda la Vodacom
Kampuni ya Vodacom ndio yenye mtandao mkubwa zaidi wa mawasiliano ya simu za mkononi katika ukanda wa ziwa Tanganyika kwa huduma zake kuwafikia wakazi wengi zaidi.
Katika kuunga mkono juhudi za serikali zenye kulenga kuongeza kiwango cha uwekezaji katika ukanda wa ziwa Tanganyika mbali na kushiriki mkutano huo Vodacom imedhamini chakula cha mchana na cha usiku kwa wajumbe zaidi ya mia nne wanaohudhuria mkutano huo.