Utalii waweza kukuza uchumi zaidi-Dk Shein

Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzbar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amesema utalii ni sekta yenye uwezekano mkubwa wa kukua na kuwa na mchango mkubwa zaidi katika ukuaji wa uchumi nchini.

Dk. Shein aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa kikao cha siku ya pili ya mkutano wa sita wa Baraza la Biashara la Zanzibar (ZBC), unaoendelea katika hoteli ya Bwawani mjini Zanzibar.

Katika hotuba yake hiyo ya ufunguzi Dk. Shein alisema kuwa kutokana na sababu hiyo, utalii umepewa nafasi kubwa katika mipango ya Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Jamii ambapo kwa mujibu wa taarifa ya mapitio ya uchumi ya mwaka 2009/2010, sekta ya utalii kwa jumla imechangia kati ya asilimia 25 hadi 27 ya Pato la Taifa.

Aliendelea kueleza kuwa sekta ya utalii inachangia asilimia 70 ya mapato ya fedha za kigeni na kusema kuwa hiyo ni dalili ya ukuaji wake ambao ulikuwa wa wastani wa chini ya asilimia 15 katika miaka ya mwanzo ya 2020.

Dk. Shein alisema kuwa ukuaji wa sekta ya utalii ni kichocho kikubwa cha ustawi wa kilimo, ajira, viwanda vidogo na vya kati na uvuvi pamoja na maendeleo ya sekta ya biashara, usafirishaji na uchukuzi wa nchi kavu, bahari na anga.

“Kwetu sisi utalii ni sekta inayofungamana na sekta nyingi nyengine kama vile uzalishaji vyakula, hasa mboga mboga na matunda”,a lisema Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Utalii pia, unachangia katika ukuaji wa ajira ambao kwa makisio ifikapo mwaka 2020, asilimia 50 ya wananchi wa Zanzibar wenye uwezo wa kufanya kazi itakuwa katika ajira zinazohusiana na utalii.

Dk. Shein alieleza kuwa kuna baadhi ya watu ambao wana hofu na sura tofauti ya utalii zikiwemo ya athari zake kwa utamaduni na kusisitiza kuwa serikali imeyazingatia hayo na ndio maana inasisitiza uhifadhi na ukuaji wa mambo yaliyo mazuri ya utamaduni wa Zanzibar katika programu mbali mbali za utamaduni na utalii.

Alieleza kuwa ni wajibu kwa wananchi kuwajuulisha watalii wanaokuja nchini juu ya utamaduni uliopo pale wanapokutana nao kaika biashara, hotelini, madukani na mitaani.

Pia, Dk. Shein alieleza kuwa athari z utamaduni hazitokani moja kwa moja na utalii peke yake bali zinatokana na utandawazi, yakiwemo maendeleo ya teknolojia na mawasiliano, kama vile tovuti, blogi na intaneti ambazo nazo huchangia kwa kiasi kikubwa.

Alisisitiza kuwa mambo hayo yanawea kuwa na uharibifu mkubwa zaidi kwa utamaduni wa Zanzibar kuliko kutokana na hoja ya watalii na kuelea kuwa la kufanya ni kuwaelimisha vijana ili wawe waangalifu zaidi.“Tutumie utamaduni wetu kama ni bidhaa itakayoleta pato kwa watu wetu”,alisema Dk. Shein.

“Serikali imeona ipo haja kuuona utalii ni muhimu na unafaida kubwa na ndio maana iatumia kauli mbiu isemayo’ Utalii ni kwa wote”,alisisitiza Dk. Shein.

Aidha, Dk. Shein alimkaribisha Rais wa Shirika la Uwekezaji la Marekani Bwana Daniel Anagho aliyeshiriki katika Mkutano huo na kutoa mada juu ya uwekezaji nchini mwao sanjari na kutoa fursa kwa wafanyabiashara wa Zanzibar na Waekezaji nchini Marekani.

Dk. Shein alieleza kuwa mahusiano ya kibiashara kati ya Zanzibar na Marekani ni ya kiaka mingi ambapo wafanyabiashara wa Marekani walianza kubadilishana bidhaa na wafanyabiashara wenzao wa Zanzibar kabla ya kufunguliwa kwa Ubalozi wa Marekani ambao uliasisi uhusiano wa kidiplomasia kati ya Zanzibar na Marekani mwaka 1937.

Alieleza kuwa Zanzibar na Marekani zilitiana Mkataba wa Urafiki wa Biashara mwaka 1933 ambapo vitambaa ilikuwa ni biashara ya mwanzo kutoka Marekani na Zazibar ilikuwa ikisafirisha pembe na viungo kupeleka Marekani hivyo, Zanzibar ilikuwa ni kituo kikubwa cha biashara katika eneo la Afrika Mashariki.

Dk. Shein alieleza kuwa Marekani ni soko la tatu kubwa kwa watalii wanaokuja Zanzibar kutoka nje , ambapo pamoja na hayo uwekezaji wa Marekani katika sekta ya utalii bado hauendi sambamba na idadi ya watalii wanaokuja nchini kutoka Marekani, hivyo utalii ni chanzo muhimu cha kufufua biashara kati ya Zanzibar na Marekani.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais Mhe. Balozi Seif Ali Idd, akimkaribisha bwana Daniel Anagho kutoka Marekani alieleza mikakati ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya utalii sanjari na kueleza haja ya mashirikiano ya uwekezaji kati ya Zanzibar na Marekani.

Balozi Seif alieleza kuwa hivi karibuni ujumbe wa uwekezaji ukiongozwa na yeye kutoka Zanzibar unatarajia kwenda nchini Marekani kwa ajili ya kuangalia maeneo ya ushirikiano kati ya Zanzibar na Mashirika ya uwekezaji ya Marekani.

Alieleza kuwa ujio wa Daniel ni kuonesha ni kwa namna gani mashiikiano yanaweza kufanyika na Makampuni ya Marekani kwani kufanya hivy kutasaidia kurejesha uhusiao wa kibiashara uliokuwepo hapo kabla kwani imeonekana hivi karibuni makampuni meng ya Marekani yamejitokeza kutafuta fursa za uwekezaji na biashara nje ya Marekani hususan katika bara la Afrika.

Nae Bwana Anagho akitoa mada yake katika mkutano huo, alieleza kuwa mashirika ya uwekezaji ya Marekani yako tayari kutoa ushirikiano na Zanzibar katika kuimarisha sekta ya uwekezaji na biashara.

Akieleza juu ya dhima kubwa ya Shirika la Uwekezaji la Afrika (AIC), alieleza kuwa ni kusaidia kuwepo kwa ubia na kushajiisha uwekezaji na ushirikiano sanjari na kufanya ushauri kwa serikali za nchi zinazoendelea kiwa ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi katika kuwavutia wawekezaji

Katika mkutano huo viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalm Seif Sharif Hamad, Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd, pamoja na wajumbe wa ZBC na wageni waalikwa mbali mbali.