Wanachama wa UWT watakiwa kuwa wavumilivu

Mke wa Rais, Mama Salma Kikwete

Na Anna Nkinda – Maelezo, Tarime

WANACHAMA wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) wametakiwa kuwa wavumilivu, na upendo, uzalendo kwa Taifa, utayari wa kuthubutu na kutenda walichokiazimia, kushikamana na kupeana moyo wakati wote wa kumkabili adui ili waweze kuwaenzi waasisi wa umoja huo.

Wito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati wa sherehe za kilele za wiki ya UWT na maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru yaliyofanyika wilayani Tarime katika mkoa wa Mara.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kuwa waasisi wa umoja huo waliongozwa na umoja, ujasiri, usikivu, kujiamini, kukubali majukumu, kuwa tayari kutumwa, moyo wa kujitolea, kushikamana na kutokukata tamaa haraka mambo ambayo yameshindwa kuenziwa na wanawake wa leo na hivyo kutokupata mafanikio kama yale ya waasisi wao.

“Kwetu sisi Mwalimu alikuwa mtu wa pekee na muhimu sana kutokana na mapenzi makubwa aliyokuwa nayo kwa wanawake na kwa kutambua siri ya nguvu kubwa za wanawake katika kufanikisha mapambano ya kuikomboa nchi yetu pia aliwaunganisha wanawake kwa kuanzisha UWT chini ya TANU chombo ambacho ni tuzo kwetu ya kutambua mchango wetu kwenye mapambano ya kudai uhuru wa nchi yetu na kwa ujenzi wa Taifa”.

“Nafarijika kuwa wanawake tunaweza, si jana wala juzi bali uwezo wetu ulianza zaidi ya miaka 50 iliyopita na bado tunaendelea jambo la muhimu ni kufanya kazi kwa bidii, upendo na moyo wa kujitolea kama ilivyo kawaida yetu tukifanya hivyo tutakuwa tumetetea maslahi yetu na jamii nzima , kwa maana mama ndiye mlezi wa familia”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alizitaja changamoto inazowakabili wanawake ambazo zinaakisi sura na majukumu ya mwanake katika jamii na hivyo kuiomba Serikali kuzitatua kuwa ni mwanamke ni shina la uhai wa jamii, kielelezo cha uhai wa Taifa, uhai wa Chama, mama wa jamii, anamiliki jamii, anawasiliana na jamii, anailea jamii na anahamasisha jamii.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa umoja huo Amina Makillagi alisema kuwa kila mwaka UWT hufanya maadhimisho ya Umoja huo, sherehe ambazo hufanyika kati ya mwezi Septemba na Oktoba ambapo katika wiki hiyo wanawake hukutana nchi nzima kukumbuka siku ambayo umoja huo ulianzishwa Novemba 2, 1978, kutathini mafanikio waliyoyapata wanawake wa Tanzania na changamoto mbalimbali zinazowakabili.

“Tuliamua kuyafanya maadhimisho haya ya UWT ya mwaka huu wa 2011 yawe maalum kwa ajili ya kutupatia fursa maalum ya kuadhimisha miaka 50 ya Uhuru, kumkumbuka na kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa kuanzisha UWT na kwa kukubali kuilea , kazi aliyoifanya hadi mwisho wa uhai wake”, alisema.

Aliyataja Mafanikio waliyoyapata tangu kupatikana kwa uhuru ni wanawake kushiriki kwenye siasa na kupiga kura wakati wa uchaguzi, ushiriki wa wanawake kwenye shughuli za uzalishaji mali, mtoto wa kike anapata fursa ya kupata elimu sawa na mtoto wa kiume, kupungua kwa mila zinazowakandamiza wanawake,kuongezeka kwa upatikana wa afya ya mama na mtoto.

Mafanikio mengine ni kurekebishwa kwa sheria zinazowakandamiza wanawake na watoto, kuimarika kwa usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake,wanawake kutotumika kama nguvu kazi ya uzalishaji.

Makillagi alisema, “Matatizo yanayowakabili wanawake hivi sasa ni kuendelea kuwepo sheria zinazowakandamiza wanawake na watoto, tatizo la mimba za utotoni na wanafunzi, upatikanaji mdogo wa maji safi na salama na umuhimu wa kuendelea kudumisha amani na utulivu nchini mwetu”.

Katibu Mkuu huyo wa UWT aliiomba Serikali kuchukua tahadhari na hatua za makusudi ili kuhakikisha kuwa amani na utulivu uliodumu nchini tokea kupatikana kwa Uhuru, unalindwa kwa gharama zote ili Tanzania iendelee kuwa kisima cha Amani na Utulivu.

Katika maadhimisho hayo tuzo mbalimbali zilitolewa kwa waasisi wa umoja huo akiwemo mama Maria Nyerere, Fatuma Karume, Hayati Bibi Titi Mohamed, Hayati Mama Sophia Kawawa, Anna Abdallah, Lea Lupembe, Dk. Msimu Abdulrahhman, Kate Kamba, , Bibi Raya wa Zanzibar na Mama Salma Kikwete kutokana na jitihada zake za kufanya kazi na kuisaidia jumuia hiyo.

Kaulimbiu ya maadhimisho hayo ambayo inalenga kuwapa wanawake fursa ya kutathimini maendeleo yao katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru ni wanawake miaka 50 ya uhuru, tumethubutu, tumeweza na sasa tunasonga mbele.