MCHEZAJI Costancia Maringa wa Tanzania ameombewa Hati ya Uhamisho wa Kimataifa (ITC) ili aweze kucheza mpira wa miguu wa wanawake nchini Ujerumani.
Chama cha Mpira wa Miguu cha Ujerumani (DFB) kimetuma maombi hayo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ili kumwezesha mchezaji huyo kuichezea timu ya FC 1919 Marnheim ya nchini humo.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa DFB, Helmut Sandrock, Maringa mwenye umri wa miaka 12 ameombewa ITC na chama hicho kama mchezaji wa ridhaa. TFF inafanyia kazi maombi hayo na hati hiyo itatolewa mara baada ya taratibu husika kukamilika.
Wakati huo huo viingilio katika mechi namba 62 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Simba na African Lyon itakayochezwa Oktoba 16 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam vimetajwa na TFF.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana viingilio hivyo vitakuwa kama ifuatavyo;
VIP A itakuwa sh. 15,000, VIP B sh. 10,000, VIP C sh. 7,000, viti vya rangi ya chungwa (orange straight and curve) sh. 5,000 wakati viti vya kijani na bluu itakuwa sh. 3,000.