Kikwete ashiriki mazishi ya Mwanahabari Penza

Rais Kikwete akimwaga mchanga kwenye kaburi la marehemu Juma Fugame Penza


RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete, Oktoba 13, 2011 aliungana na waombolezaji kumzika mwanahabari mkongwe, Juma Fugame Penza katika makaburi ya Kisutu, mjini Dar es Salaam.

Ndugu Juma Penza alifariki dunia usiku wa kuamkia jana kwenye Hospitali ya Hindu Mandal, Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 63. Marehemu Penza ambaye amekuwa katika tasnia ya habari kwa karibu miongo minne iliyopita na miongoni mwa walioshiriki mazishi yake katika makaburi ya Kisutu, Dar es Salaam ni pamoja na viongozi waandamizi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) alichokifanyia kazi kwa zaidi ya miaka 20.

Katika salamu za rambirambi ambazo Mheshimiwa Rais Kikwete amempelekea Katibu Mkuu wa CCM, Mheshimiwa Wilson Mukama na kupitia kwake kwa familia na ndugu wa marehemu, Mheshimiwa Rais amemwelezea Hayati Penza kama mwandishi wa habari aliyefanya kazi zake kwa weledi na uzalendo akiongozwa na misingi imara ya taaluma yake na uzalendo kwa nchi yake.

“Nilimfahamu binafsi Ndugu Penza wakati tulipofanya kazi pamoja katika Chama cha Mapinduzi. Hakuna shaka kuwa Marehemu Penza aliitumia taaluma yake ipasavyo, akiongozwa na weledi wa kazi hiyo na uzalendo kwa nchi yake. Kamwe, hakupata kutumia ujuzi wa kazi yake kugawa wananchi kwa misingi ya aina yoyote ile.”

Katika maisha yake, marehemu Juma Fugame alishikilia nafasi za uandamizi katika vyombo mbalimbali vya habari ikiwa ni pamoja na kuwa Kaimu Mhariri wa Mazageti ya Serikali ya Daily na Sunday News, Kaimu Mkuu wa Shirika la Habari Tanzania (SHIHATA) kabla ya kujiunga na utumishi wa CCM.

Katika utumishi huo, Marehemu Penza alipata kuwa Mwandishi wa Habari wa Katibu Mkuu wa CCM, Mzee Rashid Mfaume Kawawa ambaye pia ni marehemu, Mwandishi wa Habari wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Mzee John Malecela, Mkurugenzi wa Redio Uhuru na Afisa Mwandamizi wa masuala ya habari na vyombo vya habari katika makao makuu ya Chama.