Na Mwandishi Maalum
IRAN imetoa matrekta madogo aina ya power tiller 100 kwa Serikali ya Muungano wa Tanzania kusaidia kuinua na kuimarisha kilimo nchini na hasa kuunga mkono malengo ya Mpango wa Kilimo Kwanza.
Mchango huo mkubwa wa kusaidia kuinua na kuboresha kilimo cha Tanzania umeelezwa na Balozi wa Iran katika Tanzania, Mheshimiwa Mohsen Movahhedi Ghumi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete wakati alikutana na kufanya mazungumzo na balozi huyo.
Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Oktoba 13, 2011, Ikulu, Dar es Salaam, Balozi huyo amemweleza Rais Kikwete kuwa matreka hayo madogo yenye thamani ya dola za Marekani 600,000 yamenunuliwa kutokana na sehemu ya msaada wa maendeleo wa Iran kwa Tanzania.
Mwaka jana, Tanzania na Iran zilitiliana saini makubaliano ambako Iran iliahidi kuipatia Tanzania msaada wa maendeleo wa dola za Marekani milioni 1.2. Sehemu ya msaada huo ndiyo imetumika kununulia matekta hayo na kiasi kinachobakia cha dola za Marekani 600,000 kitatumika kujenga kliniki ya kisasa mjini Dar es Salaam kwa ajili ya kuongeza huduma za afya kwa wakazi wa jiji hilo.
Katika makubaliano hayo hayo, Iran ilikubali kutoka msaada wa dola za Marekani milioni moja kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ambako kati ya hizo kiasi kitatumika kununulia matreka madogo 50 kwa ajili ya kuendeleza kilimo Visiwani na kiasi kinachobakia kitatumika kupata boti kwa ajili ya kuimarisha shughuli za uvuvi Tanzania Visiwani.
Matreka hayo yote ambayo yanatolewa kwa Tanzania yatakabidhiwa rasmi karibuni na kiongozi mmoja mwandamizi wa Serikali ya Iran ambaye atatembelea Tanzania kwa muda wa siku mbili. Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete amemshukuru Balozi wa Iran kwa msaada huo akisema kuwa matreka hayo yatakuwa mchango mkubwa katika kufanikisha Mpango wa Kilimo Kwanza.