Na Anna Nkinda – Maelezo, Butiama
JAMII nchini imetakiwa kutowadharau, kuwanyanyasa na kuwasahau wazee bali iwaenzi na kuwathamini kwani kupitia kwao itafaidika kwa kujifunza mambo mengi zaidi ambayo haikuwa inayafahamu.
Wito huo umetolewa leo na Mke wa Rais wa kwanza na Muasisi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Hayati Abeid Aman Karume Mama Fatma Karume wakati akiongea na wakazi wa Butiama wilayani Musoma katika Mkoa wa Mara.
Mama Fatma ambaye ni mmoja wa waasisi wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) alisema kuwa baadhi ya watu katika jamii wamekuwa na tabia ya kuwadharau wazee jambo ambalo linawafanya wasifahamu mambo mengi ya zamani na hivyo kutokutambua historia ya taifa lao.
“Vijana mmejaliwa kuwa na nguvu za kutosha nawasihi mtumie vizuri akili mliyonayo kufanya kazi kwa bidii kwani wazee wenu tunaona fahari kubwa pale ambapo vijana wetu mnafanikiwa kimaisha kama ilivyo kwa wazee wenu”
Kwa upande wake Mke wa rais Mama Salma Kikwete ambaye aliambatana na Mama Karume kwa ajili ya maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru na wiki ya UWT ambayo kilele chake kinafanyika kesho (leo) katika wilaya ya Tarime alisema kuwa mchango wa wazee ulisaidia kwa kiasi kikubwa kupatikana kwa uhuru wa Tanzania.
Wakiwa katika kijiji cha Butiama UWT ulitoa msaada wa pampu ya kuvutia maji na matanki manne kila moja likiwa na ujazo wa lita 5000 ili yaweze kukabiliana na tatizo la maji katika kituo cha Afya, uliandaa dua ya kumuombea hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere iliyosomwa na vijana wa madrasa wa msikiti wa Butiama, uliandaa ibada ya misa ya kumkumbuka Mwalimu Nyerere iliyofanyika katika kanisa Katoliki Butiama pia ulitoa tuzo kwa muasisi wa Umoja huo Mama Mariam Nyerere.