MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan, amezinduwa rasmi huduma za kifedha ya kampuni ya Simu Tanzania ya ‘TTCL PESA’ inayomuwezesha wateja kupata huduma mbalimbali kama kutuma Fedha, Kulipia Ankara za huduma kama vile Maji, Umeme (LUKU), Ving’amuzi na Kununua vifurushi vya TTCL huku huduma nyingine zikiendelea kuongezwa.
Akizungumza katika uzinduzi huo, alisema uzinduzi wa TTCL PESA ni mafanikio ya kujivunia kwani itawawezesha wananchi kupata huduma za kifedha nafuu na rahisi zenye ushindani mkubwa kuendana na mahitaji ya soko. Alisema TTCL PESA itamwezesha mwananchi kutuma na kupokea fedha kwa viwango vya chini sana kupita mitandao yote nchini. Aidha aliwapongeza Kampuni ya TTCL na kuwataka kuendelea kuwa wabunifu kuongeza huduma mbalimbali katika mtandao huo ili wananchi waendelee kunufaika na ubunifu huo.
Alisema Serikali imeendelea kuiunga mkono TTCL katika hatua mbalimbali ili kuhakikisha inarejea katika hadhi yake na kutoa huduma bora kwa wananchi na kuhimili ushindani na makampuni mengine ya mawasiliano nchini. Kuwa suluhisho la kweli la utoaji huduma za mawasiliano hapa nchini.
“Uzinduzi wa huduma ya TTCL PESA ni uthibitisho mwingine wa kwamba TTCL inatekeleza kikamilifu maagizo ya Serikali ya awamu ya Tano, chini ya Rais wetu mpendwa Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ameelekeza kuwa, mashirika yote ya umma yajiendeshe kwa faida, yatoe gawio serikalini, yawahudumie wananchi kwa kiwango cha juu kabisa cha ubora na kwa gharama nafuu changamoto sokoni.” alisema Mama Suluhu Hassan.
Awali akizungumza Ofisa Mtendaji Mkuu wa TTC, Waziri Kindamba alisema kwa ujumla, ujio wa TTCL PESA itaongeza kasi ya ukuaji wa Uchumi kupitia ajira na kodi zitakazotokana na huduma hii hivyo kusaidia kusukuma agenda ya Nchi yetu ya kupiga hatua kuwa nchi ya Uchumi wa kati, Uchumi wa Viwanda hadi ifikapo mwaka 2025.
“Uzinduzi wa leo ni tukio kubwa sana, lenye uzito wa kipekee kwa TTCL na Sekta nzima ya Mawasiliano hapa nchini. Huu ni mwendelezo wa utamaduni mpya ndani ya TTCL wa kusikiliza mahitaji ya Wananchi na kutekeleza mahitaji hayo katika kipindi kifupi kadri navyo wezekana. Utamaduni wa zamani uliokuwa umezoeleka katika taasisi za Umma kuwa, taasisi hizo zinatawaliwa na urasimu wa hali ya juu katika kutoa huduma, huku zikiwasahau kabisa wateja na mahitaji yao hali iliyowavunja moyo na kuwakatisha tamaa wateja wengi.” alisisitiza Ofisa Mtendaji, Kindamba.
Hata hivyo alibainisha kuwa TTCL ya sasa inaongozwa na utendaji wa vitendo unaozingata uzalendo, uadilifu, uchapakazi na weledi katika utoaji wa huduma hivyo kuwaomba Wananchi kuiamini na kuiunga mkono katika mabadiliko hayo ya kimafanikio. Alisema TTCL ya sasa inatoka ofisini na kuwafuata wateja walipo na kuwahudumia katika muda mfupi kadri inavyowezekana kutegemeana na aina ya tatizo.
Aliongeza ujio wa TTCL PESA itawawezesha Wananchi kupata huduma mbali mbali kama Kutuma Fedha, Kulipia Ankara za huduma kama vile Maji, Umeme (LUKU), Ving’amuzi na Kununua vifurushi vya TTCL huku huduma nyingine zikiendelea kuongezwa. “Huduma za TTCL PESA zitarahisisha mchakato wa malipo kwa njia ya mtandao, zitaongeza usalama wa fedha na kupunguza hatari ya kupotea kwa fedha kupitia vitendo vya uhalifu kama ujambazi wanavyofanyiwa Wananchi (Wakulima na Wafugaji) wanaotembea na fedha nyingi katika maeneo mbali mbali wanapofanya biashara zao za mazao na mifugo.” alisisitiza Ofisa Mtendaji huyo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan (wa pili kulia) akiwa katika picha ya kumbukumbu na menejimenti ya juu ya TTCL mara baada ya kuzinduwa huduma hiyo.