KIWANJA CHA NDEGE TABORA CHATAKIWA KUJIENDESHA

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, akiwasili na ndege aina ya Bombadier Q400 ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), mkoani Tabora katika ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani humo jana.

 

Muonekano wa Taa za kuongozea ndege wakati wa kutua zilizojengewa katika Kiwanja cha Ndege cha Tabora.

 

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, ameutaka uongozi wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), kuweka mikakati endelevu ili kuwezesha kiwanja cha ndege cha Tabora kujisimamia na kujiendesha kutokana na miundombinu bora na ya kisasa inayoendelea kujengwa kiwanjani hapo.

Amezungumza hayo jana mkoani humo, mara baada ya kuanza ziara ya kikazi ambapo pamoja na mambo mengine Waziri Prof. Mbarawa amekagua na kujionea maendeleo ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho ambapo mpaka sasa ujenzi wake umefikia asilimia 96 na umegharimu kiasi cha shilingi Bilioni 27.

“Hivi sasa huduma ya usafiri wa ndege katika kiwanja hichi unaridhisha, hivyo ongezeni ubunifu ili kuvutia abiria wengi na kuwezesha kiwanja kujiendesha”, amesema Prof. Mbarawa.

 

Meneja wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja cha ndege cha Tabora Eng. Neema Joseph, akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, kuhusu maendeleo ya ujenzi yaliyofikiwa kiwanjani hapo, wakati akikagua ujenzi wake, mkoani humo jana.

 

Amesisitiza kuwa gharama za usafiri wa anga zitaendelea kupungua kadri huduma na ubora zitavyokuwa zinaendelea kuongezeka ili kuwezesha abiria wengi zaidi kutumia usafiri huo na hivyo kuwezesha pato la Taifa kuongezeka. Kwa upande wake, Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege mkoani Tabora Eng. Danstan Komba amemueleza waziri kuwa idadi ya abiria wanaotumia kiwanja cha ndege hicho imeongezeka kutoka asilimia 10 kwa mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 62.3 mwaka 2016 kutokana na ndege za ATCL kuanza safari zake mkoani humo.

Aidha, ameongeza kuwa baada ya mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho kukamilika, mashirika ya ndege yataongeza safari zake mkoani humo kwa kuzingatia uwepo wa miundombinu bora yenye kukidhi mahitaji na hivyo itatoa chachu ya maendeleo kwa wakazi wake na kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Naye, Meneja wa Mradi wa ujenzi wa kiwanja hicho Eng. Neema Joseph, amemuahidi Waziri Prof. Mbarawa kumsimamia mkandarasi kumalizia kazi zilizobaki uwanjani hapo ndani ya siku 14 na kwa kuzingatia viwango na ubora. Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amezungumza na viongozi na wafanyakazi wa Taasisi zilizo chini ya Wizara yake na kusisitiza kufanya kazi kwa kuzingatia uaminifu, weledi, kasi na uzalendo ili kuendeleza azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kuleta maendeleo kwa wananchi wake na kufikia uchumi wa viwanda ifikapo 2025.

Waziri Prof. Mbarawa yupo katika ziara ya kikazi ya siku mbili ya kukagua miradi ya miundombinu iliyopo mkoani Tabora.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano