Na Janeth Mushi, Arusha
POLISI mkoani Arusha wamekana taarifa zilizotolewa dhidi yao kuwa wamezuia maandamano ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyokuwa yamepangwa kufanyika Oktoba 9 mwaka huu.
Taarifa zilizoufikia mtandao huu zinadai kuwa Katibu wa Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Arusha Abdallaha Mpokwa, ndiye aliyeomba kusitishwa kwa maandamano, wakati jeshi hilo likiwa tayari limeshatoa kibali cha kuruhusu tukio hilo.
Akitoa ufafanuzi leo mjini hapa Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa, Leonard Paul, amesema kisheria polisi wanauwezo wa kutoa kibali kuruhusu kufanyika kwa mkusanyiko ama maandamano na hata kuzuia endapo linaona inafaa.
Amesema polisi imesikitishwa na madai hayo ya kwamba wamezuia
kibali cha kufanyika kwa maandamano ya CCM jambo ambalo si kweli.
“Maandamano hayo hatukuyazuia sisi bali wenyewe kupitia kiongozi wao
walitupigia simu na kudai kuwa wamesitisha kufanyika kwa maandamano hayo,” alisema Leonard. Kaimu huyo alidai baada ya kusitishwa kwa maandamano hayo yaliyokuwa na lengo la CCM kupongezana kama ilivyokuwa imeelekweza katika kibali walichokuwa
wameomba Chama hicho, CCM waliamua kuendelea na shughuli za ufunguzi wa matawi kama walivyokuwa wamejipanga tanga awali.
Aidha inadaiwa kuwa sababu za kuzuiwa kwa maaandamano hayo ambayo baadaye yaliruhusiwa kufanyika, ni mgogoro uliopo ndani ya UVCCM katika Wilaya ya Arusha, ambapo baadhi ya viongozi wa umoja huo wanadaiwa kupinga ziara ya viongozi hao wa kitaifa.