Meneja Mkaazi wa Kampuni ya Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee, akizungumza katika hafla fupi ya uwasilishwaji wa Ripoti ya Utalii Tanzania kwa mwaka 2017 kutoka katika kampuni hiyo inayojishughulisha na huduma za hoteli na usafiri mtandaoni tukio lililofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip katikati ya jiji la Dar es Salaam leo asubuhi.
Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Utalii Tanzania, Denis Simkoko akizungumza katika hafla hiyo.
Maofisa wa Shirikisho la Utalii Tanzania (TCT), wakiwa kwenye hafla hiyo. Kutoka kulia ni Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho hilo, Denis Simkoko, Meneja Mkuu wa Mauzo wa Hoteli ya Ramada Resort Dar es Salaam, Amina Kapya na Ofisa Tawala wa Chama cha Wamiliki wa Hoteli Tanzania (HAT), Jeniffer Abel.
Na Dotto Mwaibale
SERIKALI imeahidi kuendelea kuwashirikisha wadau mbalimbali katika sekta ya utalii hususani kwenye utungaji wa sera pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ya uendeshwaji wa shughuli hizo nchini Tanzania.
Hayo yalisemwa na Ofisa Habari na Mawasiliano wa Shirikisho la Utalii Tanzania, Denis Simkoko katika hafla fupi ya uwasilishwaji wa Ripoti ya Utalii Tanzania kwa mwaka 2017 kutoka kwa Jumia Travel, kampuni inayojishughulisha na huduma za hoteli na usafiri mtandaoni tukio lililofanyika katika ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip katikati ya jiji la Dar es Salaam leo asubuhi.
“Bila shaka mafanikio tuliyonayo kwa sasa katika sekta ya Utalii nchini ni matokeo mazuri ya ushirikiano wa karibu baina ya serikali na wadau wengine. Shirikisho la Utalii Tanzania lipo kama daraja katika kuwaunganisha wadau mbalimbali wa sekta hii nchini kote na wizara husika yenye mamlaka kwa mujibu wa serikali. Huwa tunakutana na wadau wa utalii ambapo ni takribani vyama 12 nchini kote ndani ya kipindi maalumu cha mwaka na kujadili masuala mbalimbali yanayotukabili. Baada ya hapo sasa ndiyo sisi kama shirikisho huwa tunayawasilisha maoni hayo kwa serikali ili kupata ufumbuzi na pia kutengeneza fursa ambazo zitatukutanisha pamoja wadau katika meza moja ya majadiliano, “ alisema Simkoko.
“Mbali na mchango wetu kwenye kupendekeza maboresho ya kodi na sera, pia tunao watu wetu kwenye vikosi kazi na kamati mbalimbali ambao hufanya kazi kwa ukaribu na serikali. Ingawa bado kuna changamoto katika kupata ushirikiano kamili au wa moja kwa moja baina ya serikali na sekta binafsi, bado tunaimani juu ya mifumo thabiti na ya uwazi katika uandaaji na ufanyikaji wa mikutano, majadiliano na mafunzo. Kwa kuongezea pia tunahamasisha uboreshwaji wa nyanja mbalimbali katika utolewaji wa huduma na sekta binafsi kama vile kuwekeza kwenye rasilimali watu. Kwa kushirikiana na taasisi tofauti kama vile Shirikisho la Wamiliki wa Hoteli Tanzania na Chuo cha Utalii cha Taifa tunatoa mafunzo kwa vijana kwa kuwapatia ujuzi ili waweze kuajirika kwa urahisi kwenye sekta hii nchini,” alimalizia Afisa Habari na Mawasiliano wa kutoka Shirikisho la Utalii Tanzania.
Meneja Mkaazi wa Jumia Travel Tanzania, Fatema Dharsee amebainisha kuwa maendeleo ya sayansi na teknolojia hususani kuongezeka kwa watumiaji na ueneaji wa mtandao wa intaneti umechochea kwa kiasi kikubwa kukua kwa sekta ya utalii nchini.
“Tanzania mpaka hivi sasa ina watumiaji wa intaneti zaidi ya milioni 19 kufikia mwaka 2016 kutoka milioni 17 mwaka 2015. Hilo ni sawa na ongezeko la asilimia 0.9 kwa mwaka na ueneaji wa mtandao wa intaneti wa asilimia 83 miongoni mwa watanzania milioni 50 nchi nzima. Hii ni ishara nzuri kwetu sisi Jumia Travel ukizingatia kwamba jitihada zetu kubwa ni kuhakikisha kuwa tunawawezesha watanzania kufanya huduma za hoteli na usafiri kwa njia ya mtandao. Katika ripoti yetu tuliyoiwasilisha inaonyesha kwamba idadi kubwa ya wateja wanaotafuta huduma kupitia mtandaoni inazidi kuongezeka kitu ambacho ni kizuri kwenye sekta ya utalii,” alisema Dharsee.
“Kupitia ripoti hii tumebaini kwamba idadi kubwa ya watanzania kwa sasa wanatumia simu za mkononi (asilimia 60) kutafuta hoteli mitandaoni ukilinganisha na kompyuta (asilimia 40). Lakini cha kuvutia zaidi kwenye upande wa kufanya huduma hupendelea zaidi kompyuta (asilimia 65) badala ya simu za mkononi (asilimia 35). Idadi kubwa ya hoteli zinazotafutwa na kutumiwa zaidi na wateja ni za nyota mbili (asilimia 41) na tatu (asilimia 39) ambapo bado zile za nyota moja na tano zikionyesha kutembelewa na wateja wachache kwa vigezo vya huduma hafifu (kwa zile za nyota moja – asilimia 4) na gharama kubwa (kwa zile za nyota tano – asilimia 4),” aliongezea Dharsee.
Meneja Mkaazi huyo wa Jumia Travel nchini alihitimisha kwa kufafanua juhudi wanazozifanya katika kuwawezesha wamiliki wa hoteli na wateja kuendana na mabadiliko ya teknolojia kwenye utoaji wa huduma. Ambapo kwa kiasi kikubwa karibuni kila pembe ya dunia watoa huduma na wateja wamehamia mtandaoni kwani kuna urahisi na unafuu mkubwa kwa pande zote mbili.
“Tunafanya juhudi kubwa katika kuwahamasisha wamiliki au mameneja wa hoteli pamoja na wateja kutumia zaidi huduma kwa njia ya mtandao kwani ni rahisi, gharama nafuu na ya uhakika. Kwa upande wa mahoteli tunawasaidia kwa kiasi kikubwa kuwatangaza kwa maelfu ya wateja tulionao nchini pamoja na kuwapatia mfumo rahisi wa kuendesha shughuli zao. Kwa mfano, mteja kupitia mtandao wetu amerahisishiwa kwa kupunguziwa ile adha ya kutembelea hoteli moja baada ya nyingine kwenye kutafuta ile itakayomfaa zaidi,” alihitimisha Dharsee.