NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Bara, Rodrick Mpogolo ameipongeza Benki ya NMB kwa kuanzisha akaunti ya Fanikiwa kwani ina lengo la kuwagusa watu wa kipato cha chini ambao ndiyo sehemu kubwa ya wananchi wa Tanzania. Mpogolo ameyasema hayo baada ya kutembelea banda la benki ya NMB kwenye maonesho ya Saba Saba ambapo alipata fursa ya kupata elimu kuhusu bidhaa na huduma mbalimbali zinatolewa na benki hiyo kubwa nchini.
Aidha, alisema kuwa akaunti hiyo ni nzuri kwa sababu ni mahususi kwa ajili ya wafanya biashara wadogo wadogo wakiwemo mama lishe, wakaanga chips, wauza magenge n.k ambao ni sehemu kubwa ya Watanzania. Akaunti hii pia inamwezesha mfanyabishara kutambulika kama mteja mfanya biashara, atakua mwanachama kweye klabu za biashara za NMB (NMB Business Club), itamwezesha kupata mkopo mpaka milioni thelathini, ina gharama nafuu za uendeshaji na ni rahisi kuifungua kwani haihitaji nyaraka nyingi. Lakini pia mteja anaweza kupata huduma katika matawi zaidi ya 200 ya NMB yaliyoenea nchi nzima.
“Akaunti ya Fanikiwa inalenga kuwasaidia wafanyabiashara wadogo ili waweze kukuza mitaji na kuendeleza kipato chao; mtu anapopata nafasi ya kupata mkopo ni njia ya kuongeza kipato cha familia na ndivyo uchumi wa taifa unavyoweza kujengwa, Mimi niwapongeze benki ya NMB kwa kuanzisha akaunti hii na niwahamasishe Watanzania watumie fursa hii kuweza kuongeza kipato kwa ajili ya maisha yao na waweze kukuza uchumi wa nchi yetu,” alisema Mpogolo.
Vilevile, Mpogolo aliwaasa wananchi wasiogope kuchukua mikopo kwenye mabenki ili waweze kuongeza kipato, “Ni jukumu la kila mtu kumuhamasisha mwenzake aone benki ni mahali anapoweza kupata fursa za kujikomboa kiuchumi, kuendeleza ustawi wake kwani mambo kama haya zamani hayakuwepo ambayo yanagusa watu wa hali ya chini.”
“Binafsi jambo lililonigusa ni kuanzishwa kwa akaunti ambayo inagusa watu wa kipato cha chini, naona kwamba Benki ya NMB inakwenda kuwa mkombozi wa watu wanyonge kwa kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais na serikali yake ya kuona wananchi wa kawaida na wao wanaboresha uchumi wao.”