Raia wa Liberia wajitokeza kupiga kura

Mmoja wa wagombea katika uchaguzi huo anayewania uraisi, Ellen Johnson Sirleaf

RAIA wa Liberia jana wameshiriki katika uchaguzi wa pili tangu kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo miaka minane iliopita. Shughuli ya kupiga kura inatarajiwa kuanza asubuhi hii ambapo wagombea kumi na tano wamejitokea kuwania kiti cha urais akiwemo rais wa sasa Ellen Johnson Sirleaf.

Bi Sirleaf anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa Winston Tubman wa chama cha Democratic,ambaye mgombea mwenza wake ni mcheza kandanda maarufu Gearge Weah. Mwandishi wa BBC mjini Monrovia Jonathan Paye-layleh anasema suala muhimu kwa wapiga kura ni kumpata kiongozi atakae wapa huduma bora za umeme, maji , barabara, nafasi za kazi, elimu na huduma za afya bora.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi James Fromoyan amesema tume imesambaza maafisa wa usalama kote nchini kuhakikisha kuwa kila kitu kipo sawa kwenye vituo vyote vya kupiga kura. Hata hivyo baadhi ya vyama vya upinzani havina imani kuwa tume hiyo itasimamia uchaguzi ulio huru na wa haki.

Nao raia wa Liberia ambao wanataka kuepuka ghasia sawa na zilizotokea katika nchi jirani ya Ivory Coast, wanataka mashirika ya kigeni yasimamie kwa makini uchaguzi huu ili matokeo yaweze kukubalika. Makundi mengi ya waangalizi wa uchaguzi yakiwa ni Umoja wa Afrika, jumuiya ya kiuchumi ya magharibi mwa Afrika (Ecowas), Umoja wa ulaya (EU) na shirika la carter centre linaloongozwa na aliyekuwa rais wa marekani Jimmy Carter.

Umoja wa mataifa umetuma vikosi vyake kutoka Ivory Coast na jumla ya wanajeshi na polisi elfu nane watakuwa wanashika doria kote nchini Liberia. Baadhi ya viongozi wa upinzani wamechukizwa na hatua ya kumpa Rais Ellen Johnson Sirleaf tuzo ya amani ya Nobel na wanadai kuwa hatua hiyo huenda ikawashawishi wapiga kura kumuunga mkono. Hata hivyo kamati ya Nobel imekanusha madai hayo.

-BBC