RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amezielekeza taasisi zinazohusina na chakula nchini kutumia wingi wa ziada ya chakula ulioko nchini kwa sasa kukiingiza katika masoko ya mijini ili kupunguza bei ya chakula na pia kuunga mkono jitihada za masikini wa mijini kupata chakula kwa bei nafuu.
Aidha, Rais Kikwete amezitaka taasisi hizo kuongeza kasi ya ununuzi wa chakula, na hasa mahindi kutoka kwa wakulima, ili kuwawezesha wakulima hao kuwa na nafasi ya kuweka mazao mapya yanayoanza kuvunwa kwa sasa na kukiokoa chakula hicho katika athari ya kuharibiwa kwa mvua katika baadhi ambako mvua imeanza kunyesha.
Rais Kikwete pia amezielekeza taasisi hizo kuweka mfumo rasmi wa kuwaruhusu wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kuuza chakula cha ziada katika nchi za jirani bila kuathiri upatikanaji wa chakula ama kusababisha upungufu wa chakula nchini.
Rais Kikwete ametoa maagizo hayo maalum jioni ya jana, Jumatatu, Oktoba 10, 2011, wakati alipokutana na kuzungumza na mawaziri pamoja na watendaji wa Serikali ambao taasisi zao zinahusika na upatikanaji, uuzaji na usambazaji wa chakula nchini.
Miongoni mwa walioshiriki katika kikao hicho kilichofanyika Ikulu, Dar es Salaam ni pamoja na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika Jumanne Maghembe, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkullo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, William Lukuvi. Wengine ni makatibu wakuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara ya Kilimo pamoja na maofisa wa Mamlaka ya Taifa ya Chakula cha Akiba (NFRA).
Katika mkutano wake na viongozi hao, Rais Kikwete amesisitiza kuwa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa inatumia wingi wa chakula, hasa mahindi, nchini kwa sasa kuweka chakula cha kutosha katika masoko ya mijini ili kupunguza makali ya maisha kwa ajili ya wakazi wa mjini na hasa wale wasiokuwa na uwezo mkubwa.
“Tunao wajibu wa kufumbaza (suppress) bei kwa kuingiza chakula cha kutosha katika masoko ya mijini kwa ajili ya mahitaji ya wakazi wa miji hiyo hasa wale wasiokuwa na uwezo wa kutosha kupambana na changamoto za maisha. Ni wajibu wetu kuwa na mfumo wa kuingiza chakula katika masoko yetu na kuangalia njia ya haraka ya kuwaunga mkono wakazi wa miji yetu wasiojiweza sana kwa kutumia chakula chetu cha akiba ili kupunguza ukali wa wa maisha yao,” alisema Rais Kikwete katika mkutano huo.
Kuhusu ununuzi zaidi wa chakula, Rais Kikwete amesema: “Bado kiko chakula kingi mikononi mwa wakulima wetu na naambiwa katika maeneo hasa mikoa ya nyanda za juu mvua zimeanza kunyesha mapema. Ni wajibu wetu kuhakikisha kuwa zinachukuliwa hatua za haraka kukinunua chakula hicho kutoka kwa wakulima na tukihifadhi katika mgahala yetu ya SGR.”
Kuhusu uuzaji wa chakula kwa nchi jirani na hata kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani la World Food Programme (WFP), Rais Kikwete amesema kuwa ufanywe utararibu wa kuwawezesha wafanyabiashara wetu nchini kuruhusiwa kuuza chakula cha ziada kwa nchi majirani kwa utararibu maalum na ulio wazi.
Amesema kuwa WPF wauziwe chakula kwa kadri ya mahitaji yao ili mradi uuzaji huo wa chakula kwa shirika hilo na nchi jirani ambazo zinakabiliwa na uhaba wa chakula ufanywe kwa namna ya kuhakikisha kuwa nchi inabakia na chakula cha kutosha na akiba ya chakula ya uhakika.
Rais Kikwete pia amesema kuwa watendaji wa Serikali waongeze kasi kuhakikisha kuwa baadhi ya maeneo ya mikoa ya Shinyanga na Mara ambayo yana upungufu wa chakula yanapatiwa chakula cha kutosha.
“Najua chakula kinapelekwa, lakini nataka tuongeze kasi yetu ili kuhakikisha kuwa wananchi katika maeneo hayo wanapata chakula cha kutosha hasa kwa kutilia maanani kuwa nchi sasa ina chakula cha ziada katika baadhi ya maeneo,” alielekeza Mheshimiwa Rais.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete jioni ya jana, Jumatatu, Oktoba 10, 2011, amepokea ujumbe maalum kutoka kwa Rais wa Afrika Kusini, Mheshimiwa Jacob Zuma.
Ujumbe huo uliwasilishwa kwa Rais Kikwete na Mheshimiwa Charles Nqakula, mjumbe maalum wa Rais Zuma ambaye pia ni mshauri wa siasa wa kiongozi huyo wa Afrika Kusini katika shughuli fupi iliyofanyika Ikulu, Dar es Salaam.
Mara baada ya kuwasilisha ujumbe huo maalum, viongozi hao wawili wamefanya mazungumzo kuhusu masuala ya uhusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini na yale yanayohusu kanda ya SADC na kimataifa.