Tukio hilo la kushangaza limetokea Jumamosi Juni 10,2017 majira ya saa nane mchana katika mtaa wa Mwinamila kata ya Ngokolo katika manispaa ya Shinyanga.
Mashuhuda wa tukio hilo walisema Jacob Paul ambaye ni mwenyeji wa mkoa wa Kigoma alifika nyumbani kwake leo majira ya saa saba mchana akiwa amepakizwa kwenye pikipiki na mwendesha bodaboda mwenzake huku akionekana kuwa mtu mwenye furaha kisha akaingia ndani kwake.
Walieleza kuwa baada ya takribani dakika 30 watoto wawili marehemu walifika nyumbani wakitaka kuingia ndani ya nyumba lakini mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani walijaribu kumuita lakini hakujibu ndipo wakaamua kwenda kuchungulia dirishani.
Walifafanua kuwa watoto hao walipochungulia dirishani walimuona baba yao akiwa amening’inia chumbani kisha kutoa taarifa kwa majirani na baba mwenye nyumba akaamua kutoa taarifa kwa jeshi la polisi.
“Mke wa marehemu hakuwepo tulipoona kuwa mlango ni mgumu kufunguka tuliamua kuuvunja na kumkuta amejiua na huenda chanzo cha kifo chake kimetokana na msongo wa mawazo kwa sababu tangu kutokea kwa tukio la mwendesha bodaboda Joel Gabriel Mamla (26) kufariki dunia,alikuwa anasema waendesha bodaboda wenzake wamekuwa wakimlalamikia kuwa anashirikiana na polisi kukamata waendesha bodaboda waliofanya vurugu hivi karibuni,” alieleza jirani Sarah Edward.
“Jana alikuwa anasema kuwa anapewa vitisho na wenzie kuwa anawasaliti na kusababisha waendesha wakamatwe na polisi na pikipiki zao”, alieleza jirani huyo.
“Nilikwambia mme wangu ujiuzulu uenyekiti,ona sasa waendesha bodaboda wenzako wamekuponza, wamekusababishe ujiue baba Joshua,umeacha familia yako bora, watoto hawa watalelewa na nani”, mke wa marehemu Rebeca Amos aliyekuwa analia muda wote wakati wa tukio alisikika akiongea kwa uchungu.
Alisema mme wake amekuwa akipokea vitisho kwa watu wasiojulikana wakimtuhumu kuwasaliti na kusababisha wakamatwe. Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa marehemu alikuwa analalamikiwa na waendesha bodaboda wenzake kuwa anashirikiana na jeshi la polisi kugandamiza waendesha bodaboda wenzake.
“Mwenyekiti anadaiwa kuwasaliti wenzake,hata kipindi kile mwendesha bodaboda Boaz William aliyefariki dunia kwa kugongwa gari wakati akidaiwa kuwakimbia askari wa usalama barabarani mjini Shinyanga anadaiwa kushirikiana na polisi kutorosha mwili wa marehemu na kuupeleka Kigoma kwa ajili ya mazishi ambapo hata waendesha bodaboda hawakupata hata nafasi ya kuaga mwili wa marehemu”, ilielezwa Malunde1 blog.
Diwani wa kata ya Ngokolo,Emmanuel Ntobi alifika eneo la tukio alimuomba rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuunda tume huru ya kijaji kuchunguza vifo vya waendesha bodaboda katika manispaa ya Shinyanga.
“Sasa idadi ya vifo vya waendesha bodaboda vimetokea Shinyanga, kuna utata kwani jamii inasema vifo vinasababishwa na askari polisi huku jeshi la polisi nalo likidai waendesha bodaboda ndiyo wanasababisha vifo vyao kwa kukiuka sheria za usalama barabarani, mpaka sasa pikipiki nyingi zimekamatwa”, alieleza Ntobi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi, ACP Muliro Jumanne Muliro aliyekuwepo eneo la tukio alisema wamekuta mwenyekiti huyo wa waendesha bodaboda amejinyonga kwa kutumia waya mgumu wa simu katika chumba chake.
“Tumepata taarifa kuhusu tukio hili, tulipofika tumekuta amefariki kwa kujing’iniza kwa waya, tumeuchua mwili wa marehemu kwa ajili ya kuufanyia uchunguzi hospitalini, sisi kazi yetu ni kuchunguza chanzo cha kifo, bado tunafanya uchunguzi zaidi juu ya tukio hili tutatoa taarifa zaidi baadaye,” alisema kamanda Muliro.
Tukio la mwenyekiti wa waendesha bodaboda kujiua limetokea siku tano tu baada ya jeshi la polisi mkoani Shinyanga,kulazimika kuwapiga mabomu ya machozi waendesha bodaboda, kwa kitendo cha kuundamana kupinga kifo cha mwenzao Joel Gabriel Mamla (26), kilichodaiwa kusababishwa na askari polisi PC Edmund baada ya kumkamata kwa kosa la kutovaa helmet.
Kwa mujibu wa jeshi la polisi watu 26 walifikishwa katika mahakama ya wilaya ya Shinyanga kwa mashtaka ya kufanya mkusanyiko usio halali, kufanya fujo na kujaribu kufanya maandamano kinyume na sheria.
Kati yao David Laurent alikiri kosa lake na kuhukumiwa kifungo cha miezi sita jela na wengine kesi yao iliahirishwa na itaendelea Julai 23,2017.
HII HAPA;-
TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUHUSU WAENDESHA BODABODA KUFIKISHWA MAHAKAMANI.
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA SHINYANGA KWA VYOMBO VYA HABARI TAREHE 10/06/2017
TAREHE 09/06/2017 WATU 26 WALIFIKISHWA KATIKA MAHAKAMA YA WILAYA YA SHINYANGA NA KUFUNGULIWA KESI YA JINAI NO 134 NA BAADAE KUSOMEWA MASHITAKA YA KUFANYA MKUSANYIKO USIOHALALI, KUFANYA FUJO NA KUJARIBU KUFANYA MAANDAMANO KINYUME NA SHERIA.
MAKOSA HAYO WALIYATENDA TAREHE 07/06/2017 MAJIRA YA SAA 04.30 ASUBUHI WAKATI KUNDI LA WATU WAPATAO 80 WENGI WAO WAKIWA NI WAENDESHA PIKIPIKI MAARUFU KAMA BODABODA WAKIWA ENEO LA IBINZAMATA MANISPAA YA SHINYANGA KWA PAMOJA WALIKUSANYIKA WAKAPANGA NA KUFANYA MAANDAMANO KINYUME NA SHERIA NA KUANZA KUYARUSHIA MAWE BAADHI YA MAGARI NA KUSABABISHA USUMBUFU KWA BAADHI YA RAIA NA WATUMIAJI WENGINE WA BARABARA NA HIVYO KUJENGA HOFU NA KUPELEKEA KUVUNJIKA KWA AMANI KATIKA ENEO HILO.
MTUHUMIWA MMOJA NO 18 KATIKA HATI HIYO YA MASHITAKA AITWAYE DAVID LAURENT ALIKIRI KOSA LAKE BAADA YA KUSOMEWA MASHTAKA HAYO NA MWANASHERIA WA SERIKALI CAROLINE MUSHI MBELE YA HAKIMU DENIS LUWUNGO.
MTUHUMIWA HUYO AMEHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIEZI SITA JELA NA WENGINE KESI YAO IMEAHIRISHWA NA ITAENDELEA TAREHE 23/06/2017.
WAKATI HUOHUO IMETOKEA AJALI YA PIKIPIKI NA KUSABABISHA KIFO. TAREHE 10/06/2017 SAA 08 USIKU BARABARA YA MAGANZO ENEO LA MATANDA SISI KWA SISI ZONE 1 MWENDESHA PIKIPIKI SHINJE MACHIYA MKAZI WA BUGWETO AKIWA NA PIKIPIKI NO MC 303 HUKU AKIIENDESHA KWA KASI NA BILA KUWA NA KOFIA NGUMU HELMET ALIPATA AJALI BAADA YA KUANGUKA NA KUFARIKI PALEPALE BAADA YA KUVUJA DAMU NYINGI KICHWANI.
CHANZO CHA KIFO HICHO NI MWENDO KASI , KUTOVAA HELMET NA KUPELEKEA AJALI ILIYOSABABISHA KUVUJA KWA DAMU NYINGI KICHWANI NA HATIMAYE KUFA. MWILI WA MAREHEMU UMEHIFADHIWA HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA.
IMETOLEWA NA MULIRO J MULIRO (ACP) – RPC SHINYANGA.