MPANGO WA MAENDELEO WA MWAKA 2017/18 TANZANIA
Mazingira Yanayoongoza Mpango
MHESHIMIWA Spika, Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 ni wa pili katika utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21). Msukumo wake ni kufanikisha utekelezaji wa malengo ya Mpango wa Miaka mitano hasa kwa miradi ambayo utekelezaji wake unaendelea tokea 2016/17. Mheshimiwa Spika, utayarishaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 umezingatia yafuatayo kama mwongozo: Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025; Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2016/17 – 2020/21); sera na mikakati mbalimbali ya kisekta, kikanda (EAC na SADC) na Umoja wa Afrika; Agenda ya 2030 ya Malengo ya Maendeleo Endelevu; Agenda ya 2063 ya Maendeleo ya Afrika; na Ilani ya CCM ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Vile vile, umezingatia mwenendo wa uchumi wa Taifa, kikanda na kidunia kwa mwaka 2016 na maoteo kwa mwaka 2017. Umezingatia pia hali halisi ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2016/17 na changamoto za utekelezaji zilizojitokeza. Ushirikishwaji wa Jamii katika Maandalizi ya Mpango 54.
Mheshimiwa Spika, mchakato wa maandalizi ya Mpango huu umezingatia dhana ya ushirikishi mpana wa wadau ikiwa ni pamoja na Wizara, Idara Zinazojitegemea, Wakala wa Serikali, Taasisi za Serikali, Taasisi za Utafiti na Elimu ya Juu, Sekta Binafsi na Washirika wa Maendeleo.
Pia uliweza kupata maoni ya Waheshimiwa Wabunge katika mkutano wa Tano wa Bunge la 11 kuhusu Mapendekezo ya Serikali kwa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/18. Katika mkutano tajwa, waheshimiwa wabunge walitoa maoni na mchango mkubwa uliotuwezesha kuandaa Mpango huu.
Miongoni mwa maoni mahsusi ya Waheshimiwa Wabunge ni kuwa: Ujenzi wa Reli ya Kati kwa kiwango cha standard gauge 29 upewe kipaumbele; kuboresha mazingira ya uwekezaji na kufanya biashara; utekelezaji wa mkakati wa kujenga zahanati katika kila kijiji na vituo vya afya kila kata; kuimarisha upatikanaji wa madawa na vifaa tiba; kuendeleza maeneo ya viwanda vidogo, na maeneo mahsusi ya EPZ/SEZ; kutoa kipaumbele kwa utekelezaji wa miradi ya makaa ya mawe – Mchuchuma na chuma – Liganga; kuboresha elimu ya juu na kuongeza wigo wa utoaji wa mikopo kwa wanafunzi; kuboresha miundombinu ya barabara; na programu ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Mheshimiwa Spika, maoni na ushauri wa wadau wengine ambao umezingatiwa katika maandalizi ya Mpango huu ni pamoja na: Kuimarisha ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa Mpango; upatikanaji wa mikopo ya muda mrefu na nafuu; uimarishwaji wa miundombinu msingi ya bandari na nishati ya umeme; na kuboresha utoaji wa huduma msingi za ustawi wa jamii hususan elimu, afya, maji, uboreshaji wa mipango miji, nyumba na makazi, na utunzaji wa mazingira. Shabaha na Malengo ya Uchumi Jumla kwa mwaka 2017/18
Mheshimiwa Spika, Shabaha na malengo ya uchumi jumla katika kipindi cha mwaka 2017/18 ni kama ifuatavyo:- (i) Kuongeza kasi ya ukuaji wa Pato Halisi la Taifa kufikia asilimia 7.1 mwaka 2017 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2016; (ii) Kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unabaki kwenye wigo wa tarakimu moja; (iii) Kuongeza ukusanyaji wa mapato ya ndani (ikijumuisha ya Serikali kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa) kufikia asilimia 16.5 ya Pato la Taifa; (iv) Mapato ya kodi kufikia asilimia 14.2 ya Pato la Taifa mwaka 2017/18; (v) Matumizi ya Serikali kufikia asilimia 24.9 ya Pato la Taifa; 30 (vi) Kuwa na nakisi ya bajeti (ikijumuisha misaada) ya asilimia 3.8 ya Pato la Taifa; (vii) Kuwa na akiba ya fedha za kigeni kwa kiwango kinachokidhi mahitaji ya uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje kwa kipindi kisichopungua miezi minne (4); na (viii) Kuhakikisha utulivu wa thamani ya Shilingi ya Tanzania.
Maeneo ya Kipaumbele 2017/18
Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia shabaha na malengo haya, miradi iliyobainishwa kuwa ya kipaumbele kwa Mpango wa Maendeleo wa Mwaka 2017/18 ni ile inayotarajiwa kutoa matokeo makubwa kuendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025 na Mpango wenyewe. Mingi ya miradi hii utekelezaji wake ulianza mwaka 2016/17, hivyo inaendelea. Hii ni pamoja na miradi ya: ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha Standard Gauge; Kuhuisha Shirika la Ndege Tanzania, hususan kukamilisha malipo ya ununuzi wa ndege 4; miradi ya Chuma cha Liganga na Makaa ya Mawe ya Mchuchuma; Uanzishwaji/Uendelezaji wa Kanda Maalum za Kiuchumi; Mtambo wa Kuchakata Gesi Asilia – Lindi; na Shamba la Kilimo na Uzalishaji Sukari Mkulazi. Malengo ya utekelezaji kwa maeneo haya kwa mwaka 2017/18 yameainishwa katika kitabu cha Mpango wa Maendeleo kwa Mwaka 2017/18 (Sura ya nne).
Mheshimiwa Spika, miradi mingine ya kipaumbele itakuwa katika maeneo yafuatayo: (a) Ujenzi wa Msingi wa Uchumi wa Viwanda: ikihusisha miradi ya:- Uendelezaji wa Eneo la Viwanda TAMCO – Kibaha; Tathmini ya matumizi ya eneo la Kiwanda cha General Tyre – Arusha; Mradi wa Magadi Soda – Bonde la Engaruka, Arusha; kuimarisha Mfuko wa Taifa wa Maendeleo ya Wajasiriamali (NEDF); uendelezaji wa maeneo ya viwanda vidogo katika mikoa ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Kigoma na Mtwara; ujenzi wa 31 ofisi za SIDO katika mikoa mipya.
Maeneo mengine ni pamoja na kuendeleza viwanda vya ngozi, kupanua mnyororo wa thamani wa pamba hadi nguo na uzalishaji wa madawa na vifaa tiba nchini. Kwa lengo hili, Serikali itaendelea kuhamasisha uwekezaji binafsi hususan katika viwanda vinavyotumia malighafi zinazopatikana kwa wingi nchini ikiwa ni pamoja na viwanda vya kusindika nyama, maziwa, maji, misitu, chokaa, mawe urembo, gypsum na mazao ya vyakula na matunda.
Serikali itaendelea kuziimarisha taasisi zake ili kuwekeza katika viwanda kwa njia ya PPP. (b) Kufungamanisha Ukuaji wa Uchumi na Maendeleo ya Watu: Miradi katika eneo hili ni ile inayolenga kuimarisha upatikanaji wa fursa za: Elimu na Mafunzo ya Ufundi: Kugharamia Elimumsingi bila malipo; Kupanua ruzuku na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu; Ununuzi wa vifaa kwa wanafunzi wenye mahitaji maalum; ukarabati na upanuzi wa Maktaba ya Mkoa – Dodoma; na ujenzi wa Vyuo vitano vya VETA katika Mikoa ya Geita, Simiyu, Njombe, Rukwa na Kagera. Kwa upande wa Afya na Maendeleo ya Jamii ni: hatua zitaendelezwa za kuboresha Hospitali za Rufaa na mikoa; kuhakikisha upatikanaji wa vifaa vya kisasa; kuimarisha upatikanaji wa dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi katika hospitali, vituo vya afya na zahanati; kuongeza udhibiti wa magonjwa ya kuambikiza; na kudhibiti maambukizi mapya ya virusi vya UKIMWI, hususan kwa vijana. Miradi ya Maji: ukarabati na upanuzi wa huduma za maji Vijijini; kuboresha huduma za maji katika Jiji la Dar es Salaam; mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Kahama, Nzega, Igunga, Tabora hadi Sikonge; ujenzi, ukarabati na upanuzi wa huduma za maji mijini na vijijini; na kutoa maji mto Ruvuma kwenda Manispaa ya Mtwara-Mikindani; kujenga na kuimarisha hifadhi ya vyanzo vya maji na misitu, upandaji miti, uvunaji wa maji, kuhimiza matumizi 32 ya teknolojia jadidifu na hifadhi ya mazingira. Hatua nyingine ni pamoja na kupanua upatikanaji wa maji safi, utunzaji wa mazingira, na kuimarisha uhimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi. (c) Mazingira Wezeshi kwa Uendeshaji Biashara: katika eneo hili, Serikali itaendelea na azma yake ya kupanua miundombinu ya huduma za kiuchumi kufikia azma yake ya kuboresha mazingira ya biashara ikihusisha miradi inayoendelea ya ukarabati wa miundombinu ya reli; miradi ya barabara na madaraja katika barabara za Kidahwe – Kasulu – Kibondo – Nyakanazi, Manyoni – Tabora – Uvinza, Tabora – Koga – Mpanda; Ujenzi wa barabara za juu za TAZARA na Ubungo Interchange; ujenzi wa Daraja la Selander na miundombinu ya mabasi yaendayo haraka (awamu ya II, III na IV) jijini Dar es Salaam. Aidha, miradi ya bandari ikijumuisha bandari za Dar es Salaam, Mtwara, Tanga, Bagamoyo, bandari kavu ya Ruvu na bandari za Maziwa Makuu (Victoria, Tanganyika na Nyasa). Kwa upande wa usafiri wa anga, Serikali itaendelea na ujenzi wa jengo la abiria (terminal III) katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere; upanuzi wa uwanja wa ndege wa Kigoma, Tabora na Mwanza; ujenzi na ukarabati wa viwanja vya ndege vya Geita, Sumbawanga, Shinyanga, Mtwara, Musoma, Iringa na Songea; na ukarabati wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa Kilimanjaro. (d) Kuimarisha Utekelezaji wa Mpango na Miradi: Serikali itaendelea kuchukua hatua ya kuimarisha mitaji ya benki za ndani za maendeleo (TIB na TADB) na kuanza utaratibu wa kuzitumia kama vyombo vyake vya ukusanyaji wa mikopo ya muda mrefu na ya gharama nafuu kwa wawekezaji. Aidha, eneo hili litajumuisha miradi ya kuendeleza na kusimamia matumizi ya ardhi; kuimarisha mipango miji; maendeleo ya nyumba na 33 makazi; kuweka mfumo utakaowezesha nchi kufaidika na ushirikiano wa kikanda na kimataifa; kuimarisha utawala bora na utawala wa sheria. Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ili kuchochea ushiriki na maendeleo ya sekta binafsi, hususan, sekta binafsi ya ndani, katika utekelezaji wa Mpango na ujenzi wa viwanda. Serikali itaendelea kuboresha kanuni, taratibu na mifumo ya taasisi ya usimamizi wa biashara na uwekezaji nchini. Kwa kuzingatia hili, Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na: (i) Kufanya mapitio ya sera, sheria na taratibu zinazochochea ushiriki wa sekta binafsi, ama kuwekeza moja kwa moja au kwa ubia na sekta ya umma; (ii) Kutenga maeneo ya uwekezaji ili kupunguzia sekta binafsi usumbufu hususan upatikanaji wa ardhi ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo mahsusi ya uwekezaji (EPZ, SEZ na kuanzisha land bank chini ya TIC), na kuyawekea maeneo hayo miundombinu msingi, na kuikodisha kwa wawekezaji kwa gharama nafuu; (iii) Kujenga miundombinu wezeshi (barabara, umeme, maji na reli) na kuifikisha katika maeneo ya shughuli za wawekezaji; (iv) Kusimamia utekelezaji wa sheria na taratibu na kuhakikisha kuwepo kwa amani na usalama; (v) Kuimarisha mifuko maalum ya kuchochea ushiriki wa sekta binafsi, kwa mfano SAGCOT Catalytic Fund na PPP Facilitation Fund; (vi) Kuboresha huduma kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha “one stop centre” chini ya TIC, bandari ya Dar es Salaam na vituo vya utoaji huduma ya pamoja mipakani (one stop border post); na (vii) Kuweka utaratibu utakaoboresha upatikanaji wa 34 mikopo ya muda mrefu kwa gharama nafuu ikiwa ni pamoja na kuimarisha mitaji ya benki maalum za maendeleo (TADB) na (TIB). (e) Kuhamishia Makao Makuu ya Shughuli za Serikali Kuu Dodoma: katika mwaka 2017/18 Serikali itaendelea na utekelezaji wa azma ya kuhamishia shughuli za Serikali makao makuu Dodoma. Katika utekelezaji wa azma hii, Wizara zimeelekezwa kutenga fedha za kugharamia stahili za watumishi kwa kutumia ukomo wa bajeti uliotengwa kwenye mafungu yao. Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu upatikanaji wa maeneo ya kujenga ofisi na nyumba za viongozi wa Serikali kwa kuzingatia mahitaji na maboresho ya mpango wa ardhi katika mji wa Dodoma.
Mheshimiwa Spika, kwa kuitikia wito wa Serikali wa kujenga uchumi wa viwanda, mifuko ya hifadhi ya jamii imeonesha nia ya kuwekeza katika miradi ya viwanda katika maeneo mbalimbali nchini. Baadhi ya miradi ambayo inatarajiwa kutekelezwa na mifuko hii katika mwaka 2017/18 ni pamoja na ufufuaji wa: kiwanda cha sukari katika Gereza la Mbigiri Dakawa Morogoro; kiwanda cha kutengeneza viatu katika Gereza la Karanga Moshi; kiwanda cha nguo cha urafiki; Dar Es Salaam; kiwanda cha Morogoro Canvas Mill; kiwanda cha chai cha Mponde kilichopo Lushoto Mkoani Tanga; kiwanda cha Kilimajaro Machine Tools, Kilimanjaro (KMTC) na kiwanda cha Kubangua Korosho cha Tandahimba na Newala. Vile vile, mifuko hii inatarajia kuanzisha viwanda vipya katika maeneo mbalimbali, vikiwemo: kiwanda cha dawa; kiwanda cha kuzalisha bidhaa za hospitali na gesi ya oksijeni; kiwanda cha kusindika zabibu, Chinangali Dodoma; viwanda vya kusindika nafaka na ukamuaji wa mafuta; na kiwanda cha kuzalishaji wanga kutokana na zao la muhogo na viazi vitamu huko Lindi. 35
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Miradi ya Kipaumbele yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Nne). Vihatarishi Vinavyoweza Kuathiri Utekelezaji wa Mpango 61. Mheshimiwa Spika, vipo vihatarishi mbalimbali ambavyo vinaweza kuathiri utekelezaji wa miradi ya maendeleo. Vihatarishi hivyo vinaweza kuwa vya ndani au vya nje. Kihatarishi kikuu cha ndani ni ufinyu wa rasilimali fedha na uwepo wa tofauti za mpangilio wa vipaumbele, mpango-kazi na mtiririko wa upatikanaji fedha baina ya taasisi za utekelezaji. Vihatarishi vya nje ni pamoja na: mitikisiko ya kiuchumi kikanda na kimataifa; majanga asilia na athari za mabadiliko ya tabianchi; na mabadiliko ya kiteknolojia.
Mheshimiwa Spika, Serikali kwa kushirikiana na wadau katika kutekeleza Mpango huu, imebainisha na kuweka tahadhari kwa kuchukua hatua zifuatazo:- kuandaa bajeti yenye mwelekeo wa kupunguza utegemezi wa kibajeti kwa kuwianisha vyanzo vya mapato na mkakati wa kuyakusanya na kuwianisha matumizi na upatikanaji wa mapato ya Serikali; kuboresha mazingira ya biashara kwa lengo la kuimarisha sekta binafsi kuchangia utekelezaji wa baadhi ya miradi; na kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu Mpango na namna bora ya utekelezaji ili kuongeza ushiriki wa jamii na sekta binafsi. Ugharamiaji wa Mpango 2017/18 Sekta ya Umma
Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/18, Shilingi bilioni 11,999.6 zimetengwa kwa ajili ya kugharamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ambapo Shilingi bilioni 8,969.8 ni fedha za ndani na Shilingi bilioni 3,029.8 ni fedha za nje. Hivyo, fedha zilizotengwa katika bajeti ya maendeleo zimeongezeka kutoka Shilingi bilioni 11,820.5 mwaka 2016/17 hadi Shilingi bilioni 11,999.6 kwa mwaka 2017/18, ikiwa ni 36 sawa na asilimia 38 ya bajeti yote. Kiasi hiki ni kikubwa kwa asilimia 1.2 ya makadirio ya kutenga Shilingi bilioni 11.80 kila mwaka kutoka mapato ya Serikali kama ilivyojidhihirisha katika mapitio ya utekelezaji kwa mwaka 2016/17. Serikali itahakikisha kuwa kiasi cha fedha kilichopangwa kwa matumizi ya maendeleo kinapatikana na kugawiwa kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo iliyokusudiwa na kwa wakati. Hivyo, pamoja na juhudi za kupanua na kukusanya mapato katika vyanzo vya kawaida vya Serikali, msisitizo umewekwa katika kubaini na kukusanya kutoka vyanzo vipya.
Mfumo wa ukusanyaji katika baadhi ya maeneo utafanyiwa mabadiliko ili kuongeza ufanisi. Mashirika na Taasisi za Umma 64. Mheshimiwa Spika, katika historia ya nchi yetu na pia nchi nyingi zinazoendelea, Mashirika ya Umma yamekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia maendeleo ya nchi husika. Kwa kutambua hili, Serikali imeelekeza mashirika na taasisi zake za umma za kibiashara kuchangia katika kugharamia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini. Taasisi hizi zinaweza kutekeleza hili kupitia mapato na/au kwa kukopa kwa ridhaa ya Serikali kutokana na dhamana ya mali zao ili kugharamia utekelezaji wa miradi itakayobainishwa kuwa ya kipaumbele. Sekta Binafsi
Mheshimiwa Spika, kama ilivyojidhihirisha mwaka 2016/17, sekta binafsi, ya ndani na nje, imepokea kwa hamasa wito wa Serikali wa kuchochea uwekezaji hasa katika maeneo mengine zaidi ya kilimo na madini. Serikali kupitia Baraza la Taifa la Biashara itaendelea kusimamia utekelezaji wa maazimio yenye lengo la kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji na uendeshaji biashara nchini. Katika kuvutia uwekezaji kwa njia ya ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, Serikali itaendelea kuimarisha Mfuko wa fedha wa miradi ya ubia (PPP Facilitation Fund) kwa lengo la kugharamia 37 uandaaji wa upembuzi yakinifu kwa miradi inayotarajiwa kutekelezwa kwa njia ya ubia kati ya Serikali na sekta binafsi. Matokeo tarajiwa ni ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi katika miradi ya kipaumbele kwa njia ya ubia. Serikali pia imeamua, kwa makusudi kuondoa mlolongo wa kodi kwa sekta ya kilimo na biashara ndogo ndogo kwa ajili ya kuinua uwekezaji katika sekta hizi. Vile vile, imechukua hatua za kuhakikisha upatikanaji wa maeneo ya viwanda na biashara ndogo kwa urahisi. Msukumo pia umewekwa kuboresha upatikanaji wa mikopo ya gharama nafuu na ya muda mrefu kwa wawekezaji, ikiwa ni pamoja na kuimarisha benki za maendeleo nchini.
Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Ugharamiaji wa Mpango yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Tano). Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji wa Taarifa 67. Mheshimiwa Spika, moja ya changamoto za utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo ni udhaifu katika ufuatiliaji wa miradi. Udhaifu huu unatokana na changamoto za upatikanaji wa rasilimali fedha pamoja na upungufu wa watumishi wenye uzoefu na utaalam wa ufuatiliaji na tathmini.
Mheshimiwa Spika, Serikali katika kuimarisha eneo hili imeamua kuweka mfumo wa mafunzo na malezi yatakayoharakisha kuimarisha utaalam wa kupanga, kutayarisha, kusimamia, kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi. Ninatumia fursa hii kuwaelekeza Maafisa Masuhuli kutenga fedha za ufuatiliaji na tathmini kama sehemu ya gharama za utekelezaji wa miradi husika.
Mheshimiwa Spika, hatua pia zimechukuliwa kwa lengo la kuhuisha nyenzo za ufuatiliaji na tathmni. Hii ni pamoja na 38 kuandaa na kutoa mafunzo juu ya matumizi ya Mwongozo wa Usimamizi wa Uwekezaji wa Umma. Kwa mwaka 2017/18, mafunzo yatatolewa kwa maofisa wa ufuatiliaji na tathmini kuwawezesha kujua hatua za msingi katika kuandaa, kuratibu na kutathmini miradi ya maendeleo. Serikali kupitia Tume ya Mipango itaandaa mfumo wa kuhifadhi taarifa za miradi ya maendeleo kwa ajili ya kuimarisha upatikanaji wa taarifa za ufuatiliaji na tathmini.
Mheshimiwa Spika, kwa lengo la kuimarisha vigezo vya kufuatilia na kutathmini utekelezaji wa miradi, Serikali kupitia Tume ya Mipango itaratibu zoezi hilo kupitia Mkakati wa Utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Hatua hii itasaidia kuboresha upatikanaji wa taarifa za ufuatiliaji na tathmni ya miradi husika kwa kuzingatia vigezo vya utekelezaji vilivyokusudiwa kwa kipindi husika. 71. Mheshimiwa Spika, maelezo ya kina kuhusu Ufuatiliaji, Tathmini na Utoaji Taarifa yapo katika kitabu cha Mpango (Sura ya Sita).
MAJUMUISHO NA HITIMISHO
Majumuisho
Mheshimiwa Spika, tangu Serikali ilipotangaza dhamira ya kujenga uchumi wa viwanda kumekuwa na mwitiko wa uwekezaji, wa umma na binafsi, unaotia matumaini makubwa. Jitihada hizi hazina budi kuungwa mkono, hususan, kwa kuweka kusudio la kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na uendeshaji biashara nchini. Hivyo, hatua za mapitio ya sera, sheria, kanuni na mfumo taasisi wa usimamizi zitaendelea kuimarishwa ili kuhakikisha kuwa tunakuwa na mfumo unaoakisi kusudio hili kwa vitendo. Aidha, hasa kutokana na ukweli kuwa sehemu kubwa ya viwanda vitakavyoanzishwa vitatumia malighafi zinazopatikana kwa wingi hapa nchini, hatua za makusudi zitaendelea kuchukuliwa kwa lengo la kuongeza uzalishaji, tija na ubora wa malighafi 39 zinazozalishwa nchini ili kukidhi mahitaji ya soko linalozidi kukua na kubadilika.
Mheshimiwa Spika, kuna kasi kubwa ya mabadiliko ya mfumo wa maisha na matarajio ya jamii, hasa kundi kubwa la vijana. Matarajio haya ya vijana yanaweza kufikiwa tu ikiwa wataweza kuajiriwa au kuwa na shughuli za kujiajiri wenyewe. Kwa mantiki hii ni wajibu wa msingi kabisa wa Serikali kuzidi kupanua fursa za uwekezaji. Uwekezaji unaweza kuwa ama wa Serikali moja kwa moja, ubia kati yake na sekta binafsi au wa sekta binafsi moja kwa moja. Kwa kutambua hili, Serikali inahitaji sana ushirikiano na mshikamano kati yake na sekta binafsi.
Ushirikiano na mshikamano huu unapaswa kuwa mpana na wa kina katika nyanja zote, kuanzia kuibua, kupanga, kutekeleza na kufuatilia na kutathmini hatua za utekelezaji. Katika kutekeleza hilo, msukumo umewekwa katika kuimarisha ushirikiano na sekta binafsi kwa kuandaa mikutano na mashauriano ya mara kwa mara ikiwa pamoja na ya Baraza la Biashara Tanzania (TNBC) itakayojadili na kutoa mapendekezo ya namna ya kuondoa changamoto zilizopo.
Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Tano ilitangaza toka mwanzo kabisa azma yake ya kujitanabaisha kuwa ya ukweli na uwajibikaji hasa katika kusimamia matumizi ya rasilimali zinazopatikana kwa manufaa ya Taifa na kila mwananchi. Kutokana na hili, Serikali inaendelea kujielekeza katika kuimarisha makusanyo ya mapato ya ndani kwa kufanyia mapitio ya mifumo na muundo wa usimamizi wa makusanyo ya kodi, malimbikizo ya kodi, kupanua wigo wa kodi kwa kusajili walipa kodi wapya, pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kuongeza makusanyo ya kodi. Msukumo pia umewekwa katika kuongeza matumizi ya teknolojia ya kielektroniki ili kupunguza athari za mapungufu ya kibinadamu katika kukusanya, kutunza na kuhifadhi fedha na kumbukumbu. Hatua hizi zote ndizo zitawezesha ustawi wa uchumi na utekelezaji bora wa Mpango wa Maendeleo. 40
Mheshimiwa Spika, mafanikio yaliyopatikana katika uchumi na utekelezaji wa Mpango yamechangiwa na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo nchi marafiki, washirika wa maendeleo, sekta binafsi na wananchi kwa ujumla. Kwa niaba ya Serikali, ninawashukuru wadau hao kwa michango yao.
Mheshimiwa Spika, kabla ya kumaliza hotuba yangu napenda kumshukuru Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu K. Kijaji (Mb), Mawaziri na Makatibu Wakuu wa Wizara zote, Wakuu wa Idara za Serikali na Taasisi zinazojitegemea kwa ushirikiano wao wakati wote wa maandalizi ya kutayarisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18. Kipekee napenda kuwashukuru watendaji wote wa Wizara ya Fedha na Mipango wakiongozwa na Katibu Mkuu Bw. Doto James kwa kusimamia vizuri kazi za kila siku za Wizara. Aidha, niwatambue Bw. Maduka Kessy, Kaimu Katibu Mtendaji, viongozi na watumishi wote wa Tume ya Mipango kwa kufanikisha maandalizi ya hotuba hii.
Hitimisho
Mheshimiwa Spika, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwa kunisikiliza. Aidha, hotuba hii na vitabu vya Hali ya uchumi 2016, na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18 vinapatikana katika tovuti ya Wizara ya Fedha na Mipango www.mof.go.tz na www.mipango.go.tz. 78. Mheshimiwa Spika, baada ya maelezo hayo naomba sasa Waheshimiwa Wabunge wapokee, kujadili na kupitisha Taarifa ya Hali ya Uchumi 2016 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2017/18. 79. Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.