WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe leo ametuma ubani na salamu za rambirambi kwa familia ya msanii mkongwe katika fani ya uchoraji Mzee Francis Maige Kanyasu (86), kufuatia kifo cha msanii huyo kilichotokea jana tarehe 29 Mei, 2017 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Waziri Mwakyembe ametuma ubani na salamu hizo za rambirambi leo mchana kupitia kwa Mtendaji Mkuu wa Baraza la Sanaa la Taifa, Godfrey Mngereza, ambaye vilevile amemwelekeza kushirikiana kwa karibu na ndugu na jamaa wa marehemu katika mazishi yake.
Katika salamu zake za rambirambi, Waziri Mwakyembe amesema Wizara itahakikisha michango ya wasanii wakongwe kama Mzee Kanyasu, inafuatiliwa kwa karibu na kuwekewa kumbukumbu kwa faida ya vizazi vijavyo.
Kufuatia taarifa iliyotolewa na Hospitali ya Taifa Muhimbili, hali ya mzee Francis ilibadilika ghafla wakati alipokuwa akipatiwa huduma ya matibabu hospitalini hapo hivyo kupelekea mauti yake.
Bwana alitoa na Bwana ametwaa, jina lake lihimidiwe.
Imetolewa na: Genofeva Matemu
Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo
30/05/2017