Na Benedict Liwenga-WHUSM, Moshi
KIWANDA cha Utengenezaji Vipuri vya Mashine Kilimanjaro (KMTC) iko mbioni kujenga mtambo utakaotumika katika kuyeyusha chuma kwa ajili ya kuendeleza shughuli zake za utenegenezaji wa dhana mbalimbali za mashine ikiwemo kukarabati mifumo ya umeme ya kiwanda hicho ambaye ilikua haijatumika kwa muda mrefu.
Kauli hiyo imetolewa jana na Meneja Mkuu wa Kiwanda hicho, Mhandisi Adriano Nyaluke wakati alipokutanana Waandishi wa habari na kueleza mikakati ya kukiendeleza kiwanda hicho ikiwemo shughuli mbalimbali zinazofanyika kiwandani hapo ili baadaye kiweze kutoa ajira rasmi kwa Watanzania.
MhandIsi Nyaluke amesema kwamba, kwa sasa katika amamu ya kwanza wana mahitaji ambayo yanahitajika kukamilika ikiwemo mpango wa kutafuta fedha toka katika Mifuko ya Jamii ili kuweza kujenga mtambo huo pamoja na fedha za mtaji wa kutengeneza zana mbalimbali kiwandani hapo.
“Mpaka sasa tuna bajeti ya shilingi bilioni 1.6 na tuna mpango wa kuendelea kutafuta fedha zaidi toka katika Mifuko ya Kijamii na tunaamini fedha hizo tutazipata ili tuweze kuendelea na mpango wa kujenga mtambo huo pamoja na utengenezaji wa zana za kiwanda”, alisema Nyaluke.
Ameongeza kuwa, hapo awali kiwanda kilijipanga kuwa na sehemu kuu mbili ikiwemo sehemu ya kuyeyusha chuma na nyingine ni sehemu ya kuchongea vipuri mbalimbali vya mashine (Mashusho) lakini mpaka 1984 sehemu iliyokuwa imejengwa ni ya kuchongea vipuri tu, hivyo mtambo wa kuyeyusha chuma ulikuwa bado haujakamilika ndiyo maana kwa sasa lengo kubwa ni kufanya maandalizi ya kuujenga mtambo huo.
“Kwakuwa mtambo wa kuyeyusha chuma ulikuwa bado haujajengwa mpaka 1984, ilibidi baadhi ya malighafi za chuma zitoke nchini Bulgaria hivyo hapa tulikuwa tunazifanyia uunganishaji na umaliziaji yaani uchongaji na upakaji rangi (Finishing and assembling) kuanzia 1984 hadi 1992”, aliongeza Nyaluke.
Aidha, amefafanua kuwa, sababu kubwa iliyokifanya kiwanda hicho kufungwa Desemba 1998 kulitokana na uhaba wa malighafi kwa ajili ya kiwanda, lakini baadaye Serikali ikatafuta Mwekezaji ambaye angeweza kukiendeleza kiwanda hicho lakini mpaka 2006 hakupatikana ndipo ikaamua kukifufua upya ili kiendelee na uzalishaji na mwaka 2008 kikakabidhiwa kwa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).
Mhandisi Nyaluke ameeleza pia, katika kukifufua kiwanda hicho, iliwekwa mipango ya kiwanda kuweza kutengeneza vifaa ambavyo hapo awali vilikua vinaagizwa toka Bulgaria na ndiyo maana mpango wa kujenga mtambo wa kuyeyushia chuma ulipangwa, mpango mwingine ni utafutaji wa soko la vifaa vinavyohitajika nchini.
Amebainisha shughuli mbalimbali wazifanyazo kiwandani hapo ikiwemo mashine za kuchonga vyuma, mashine za kuchonga maumbo mbalimbali ya vyuma, mashine za kukata vyuma, mashine za kutoboa, mashine za uselemala kama vile randa, mashine za kukata mbao pamoja mashine za kukereza na kuchonga mbao.
“Eneo kubwa tuliloona linahitaji mashine zaidi nchini ni eneo la kusindika mazao mbalibali kama vile mashine za kusaga mazao, mashine za kukamua mafuta, za kusindika matunda na mpango wa mwanzo tuliona kwa miaka mitano ya kwanza tunaweza kutengeneza mashine mbalimbali zipatazo 700 ambazo zitauzwa hapa nchini na nyingi ni za kusindika mazao, ujenzi na mashine za uchimbaji madini migodini”, aliongeza Mhandisi Nyaluke.
Kuhusu suala la ajira kiwandani hapo, amefafanua kuwa, ajira watatoa ingawa sio kwa kiasi kikubwa kwasababu bado uzalishaji sio mkubwa lakini ajira kubwa ni zile zitokanazo na mashine zinazotengenezwa kiwandani hapo.
Ameeleza kuwa, kwa sasa wamepanga awamu mbalimbali za kukifufua kiwanda hicho ikiwemo ya kwanza itayochukua miaka miwili ya kutafuta fedha za kuunda mtambo wa kuyeyusha chuma, ya pili ni ya kuendelea kutengeneza vipuri vya mashine kiwandani hapo ili kuongeza bidhaa zaidi na ya tatu ni ndiyo ya ujenzi wa mtambo huo mkubwa wa kuyeyushia chuma.
Kiwanda cha KMTC kilianzishwa kwa ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Bulgaria mnamo mwaka 1980 hadi 1983 na kilianza kufanya kazi 1984 ambapo dhumuni la kuanzishwa lilikuwa ni kutengeneza mashine zitakazotumika kutengeneza mashine za uzalishaji mbalimbali ikiwemo zana za kilimo, samani na dhana nyingine muhimu kama vile vipuri vya uzalishaji viwandani ambapo kwa sasa kampuni hiyo iko chini ya Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC).