Na Jumia Travel Tanzania
HIVI ushawahi kujiuliza ni kwanini hoteli fulani inatajwa kuwa ni ya nyota tatu, nne au tano? Najua itakuwa ni vigumu kuelewa kama haupo katika tasnia ya masuala ya hoteli au utalii mpaka upatiwe ufafanuzi wa kutosha.
Hivi karibuni Serena Hotel ya jijini Dar es Salaam ilifanikiwa kupewa hadhi ya kuwa hoteli ya nyota tano katika hafla ambayo mgeni rasmi alikuwa ni Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe.
Umuhimu wa kuzipatia hadhi hoteli husaidia sana kuchochea ushindani katika biashara hasa kwa upande wa uboreshaji wa huduma.
Kupitia makala haya Jumia Travel imekukusanyia vigezo ambavyo mara nyingi huzingatiwa mpaka hoteli kupewa hadhi fulani. Nyota moja. Mara nyingi hoteli hizi humilikiwa na watu binafsi katika utoaji wa huduma za malazi kwa wateja. Huwa ni ndogo na za ukubwa wa saizi ya kati zikipatikana katika maeneo ambayo gharama za maisha ni ya kawaida kabisa.
Kikubwa kinachozingatiwa ni kuweza kukidhi mahitaji ya msingi kwa gharama nafuu. Baadhi ya huduma zinazopatikana ni pamoja na mapokezi, kiti, meza, simu, luninga vyumbani, bafu na usafi wa kila siku. Ni chache zenye migahawa kwa ajili ya chakula, mbali na hapo huduma na mhudumu kwa vyumbani huwa hakuna.
Kwa hapa nchini Tanzania nyingi huwa ni nyumba za kulala wageni. Mfano wa hoteli hizi ni kama vile Perfect Hotel na Sharon House Hotel. Nyota mbili. Hoteli za namna hii hazina tofauti sana za nyota moja kwani nazo zinapatikana kwenye maeneo ambayo gharama za maisha ni za kawaida pia.
Mazingira na vitu vyake kama vile samani ni vya kawaida lakini vikiwa katika hali nzuri na safi. Asilimia kubwa huwa na huduma ya kifungua kinywa lakini si mgahawa. Pia zipo karibu na maeneo ambayo mteja anaweza kupata chakula kwa gharama nafuu. Wateja wanaweza kwenda muda wowote ingawa kuna ukomo ikifika muda fulani kama vile labda kuanzia saa tano usiku. Mfano wa hoteli hizi ni kama vile Golden Coins Hotel na Four Points Hotel.
Nyota tatu. Kwa kawaida hoteli za aina hii hutoa huduma ya vyumba vizuri, vikubwa vikiwa na mapambo ya kuvutia.
Hupatikana katika maeneo makuu ya kibiashara na ya kisasa pamoja na maduka kwa ajili ya mununuzi. Huwa na mgahawa unaotoa huduma ya chakula kuanzia asubuhi mpaka usiku na dawati la mapokezi huwa wazi kwa takribani masaa 14. Mbali na hayo, mteja hufikishiwa huduma mpaka chumbani, maegesho ya magari, huduma ya kubebewa mizigo inapohitajika, sehemu ya kufanyia mazoezi na bwawa la kuogelea pia huwa vinapatikana. Mfano wa hoteli hizi ni kama vile Keys Hotel Moshi na Kilimanjaro Wonders Hotel.
Nyota nne. Mara nyingi hoteli zenye hadhi hii huwa kubwa. Zina mandhari nzuri kuwavutia wageni, huduma ya mapokezi ambapo lugha zaidi ya moja inazungumzwa na wabeba mizigo kwa ajili ya wateja pia wapo. Hupatikana kwenye maeneo yaliyo karibu na hoteli zenye hadhi sawa na zao vilevile karibu na maduka makubwa ya manunuzi, sehemu za chakula na mandhari yenye vivutio vya hali ya juu.
Huduma ni zenye ubora mkubwa, vyumba vya kisasa na samani za kupendeza. Huwa na mgahawa wenye vyakula zaidi ya aina moja kwa machaguo ya wateja wa aina tofauti na pia huduma ya mteja kuhudumiwa hata akiwa chumbani kwake hupatikana.
Hoteli zingine hutoa huduma ya kuwaegeshea magari au matengezo wateja wa pamoja na kuwasaidia na usafiri wa ndani ya eneo alilofikia. Kwa kuongezea, sehemu ya kufanyia mazoezi, bwawa moja la kuogelea au zaidi pia kawaida kupatikana kwenye hoteli za namna hii. Mfano wa hoteli hizi ni kama vile Gold Crest Hotel na Ramada Resort Dar es Salaam.
Nyota tano. Hizi ni hoteli ambazo hutoa huduma za malazi na nyinginezo katika kiwango cha hali ya juu kabisa. Huwa na huduma kwa wateja binafsi zenye ubora wa
kipekee.
Ingawa mara nyingi hoteli za namna hii huwa ni ushirikiano wa makampuni makubwa lakini pia baadhi ya watu wachache huweza kutoa huduma sawa au kuzidi ushirika au makampuni
makubwa. Maeneo zilizopo hutofautiana kutoka maeneo maalum au kuwa katikati au
kitovu cha jiji kwenye shughuli nyingi za kibiashara.
Unaweza kukuta hoteli ina migahawa mpaka mitatu na yote ikiwa na vyakula vya aina tofauti. Huduma mpaka vyumbani ni masaa 24 kwa kawaida pamoja na nyinginezo lukuki ambazo mteja atazihitaji. Mfano wa hoteli hizi ni kama vile Singita Sasakwa Lodge na Essque Zalu Zanzibar.
Kwa ujumla vipo vigezo vingi tu ukiachana na hivyo vichache viliyotajwa hapo juu.
Mitandao na mashirika kutokea nchi mbalimbali imejaribu kufafanua na kuorodhesha kwa mujibu wa mahali walipo.
Hivyo basi vigezo ambavyo vinatumika hapa Tanzania vinaweza visitumike au vikawa tofauti na kwingineko.