Meneja Masoko wa kampuni ya Sun King nchini Tanzania, Albert Msengezi, akizungumza na wanahabari kwenye uzinduzi rasmi wa ofisi na bidhaa za Sun King nchini, uliofanyika hii leo Buzuruga Plaza Jijini Mwanza.
Mkuu wa Masoko wa kampuni ya Sun King Tanzania, Judie Wu, akizungumza kwenye uzinduzi rasmi wa ofisi na bidhaa za Sun King nchini Tanzania, uliofanyika Buzuruga Plaza Jijini Mwanza hii leo.
Mgeni Rasmi, Afisa Tawala wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza, Zubeda Kimaro, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, kwenye uzinduzi rasmi wa ofisi na bidhaa za Sun King nchini Tanzania, uliofanyika Buzuruga Plaza Jijini Mwanza hii leo.
Na George Binagi
WAKAZI wa maeneo ambayo bado hayajafikiwa na huduma ya umeme nchini, wanatarajiwa kunufaika na huduma hiyo kupitia mitambo ya umeme wa jua kwa bei nafuu inayosambazwa na kampuni ya Sun King.
Meneja Masoko wa kampuni hiyo nchini, Albert Msengezi, ameyabainisha hayo hii leo Jijini Mwanza kwenye uzinduzi rasmi kitaifa wa bidhaa za Sun King ambazo ni taa za sola pamoja na majiko bunifu ya Jikokoa.
“Kila Kijiji nchini tunakusudia kuwa na mawakala wa kampuni ya Sun King ambao watawafikia wananchi wote wanaoishi katika maeneo hayo na hadi kufikia mwishoni mwa mwaka huu tunakusudia kuwa na wanufaika zaidi ya Milioni Moja ambapo tumejikita kwenye bidhaa bora zisizochafua mazingira ikiwemo taa za sola na majiko yasiyochafua mazingira”. Amebainisha Msengezi.
Mkuu wa Masoko wa kampuni ya Sun King, Judie Wu, amesema kampuni hiyo imedhamiria kuhakikisha kila mmoja Mjini na Vijijini anapata huduma ya umeme pamoja na kutumia majiko bunifu yasiyo na madhara kiafiya kwa bei nafuu.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kwenye uzinduzi huo wa bidhaa za King Sung, Zubeda Kimaro ambaye ni Afisa Tawala wilayani Nyamagana, amewahimiza wawekezaji kujitokeza kwa wingi kuwekeza mkoani Mwanza kwani kuna fursa nyingi za kiuwekezaji hatua ambayo pia itazalisha ajira zaidi kwa vijana.