Pumzika kwa Amani Isango Wangu…!

Josephat Isango enzi za uhai wake.

NIMEPOKEA kwa mstuko mkubwa taarifa ya kifo cha mwandishi wa habari mwenzetu na aliyekuwa mfanyakazi wa kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited (HHPL), Josephat Isango, kilichotokea asubuhi ya leo, tarehe 14 Aprili 2017.

Nilianza kufahamiana na Isango wakati akiwa mchangiaji wa makala katika magazeti mbalimbali na baadaye akajiunga na gazeti la Tanzania Daima. Namfahamu kama mchapakazi, mwadilifu na mkweli. Alikuwa anashindana kwa hoja.

Yeye ni mmoja wa waandishi wachache nchini walioamini kwamba maadili ya uandishi hayatungwi na serikali wala wanasiasa wenye uchoyo wa kuandikwa kwa mapambo, bali wanataaluma wenyewe.

Alikuwa mmoja wa waandishi mahiri wa magazeti yanayochapishwa na kampuni yetu ya MwanaHALISI, MSETO, MAWIO, MwanaHALISI Online na MwanaHALISI Forum.

Hata pale alipoacha kazi na kuondoka HHPL, Januari mwaka huu, bado aliendelea kuchangia maendeleo ya kampuni hii, hadi mauti yanamkuta.

Niliongea naye kwa simu mara ya mwisho Jumapili iliyopita, wakati akiwa nyumbani kwao Singida, mimi nikiwa njiani naelekea Dodoma.

Ni katika mazungumzo yetu hayo, ndipo aliponieleza kuwa alikuwa anasumbuliwa na moyo, jambo ambalo lilikuwa linasababisha kushindwa kupumua vizuri.

Wakati wa uhai wake, tulifanya kazi bega kwa bega na kuna wakati nilikuwa nampigia simu usiku wa manane Isango kumweleza kuhusu habari ambayo tulipaswa kuijadili, kesho yake alifika ofisini saa moja asubuhi.

Kwa kweli, alikuwa na bidii sana na kazi. Alikuwa tegemeo kwa kampuni na pengo alilotuachia, ni vigumu kuliziba.

Isango atakumbukwa kutokana na ujasiri wake wa kuandika kile ambacho watawala walikuwa hawakipendi na; au hawataki kiandikwe.

Kuna mengi ya kuelezwa juu ya Isango. Lakini yatosha kusema, sisi tulimpenda, lakini Mungu amempenda zaidi.

Hivyo basi, nachukua nafasi hii, kutoa pole kwa wafanyakazi wa HHPL, mke wake mpendwa, familia, ndugu jamaa na marafiki, kwa kuondokewa na kipenzi chetu.

Aidha, natoa pole kwa mwenyekiti wa taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe kwa kuondokewa na kada wake mahiri na ambaye mwaka 2010, aligombea ubunge katika jimbo la Singida Mjini.

Huwezi kuzungumzia kukua na kushamiri kwa Chadema, bila kutaja mchango wa Isango. Kuna wakati Isango huyu alikuwa akitumwa kufanya kazi za kampuni iliyomuajiri, lakini aliziacha na kufanya kazi za Chadema.

Ni kweli Isango umeondoka, lakini siwezi kukusahau. Nitaendelea kukumbuka na kukuenzi kwa kuwa nilikufahamu na kukupenda. Pumzika salama Isango.

Saed Kubenea,
Mkurugenzi Mtendaji wa HHPL.