RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa mshtuko na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya Askari Polisi 8 waliouawa kwa kushambuliwa na watu wenye silaha jana jioni tarehe 13 Aprili, 2017 katika eneo la Jaribu Mpakani, Wilaya ya Kibiti Mkoani Pwani.
Askari Polisi hao walikuwa wakitoka kubadilishana doria na wameshambuliwa kwa kupigwa risasi wakiwa wanasafiri kwa gari katika barabara ya Dar es Salaam – Lindi. Mhe. Rais Magufuli amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP-Ernest Mangu, familia za askari wote waliouawa, Askari Polisi wote na Watanzania wote walioguswa na vifo hivyo.
“Nimeshtushwa na nimesikitishwa sana na vifo vya askari wetu 8 ambao wamepoteza maisha wakiwa wanalitumikia Taifa, naungana na familia za marehemu wote, Jeshi la Polisi na Watanzania wote katika kipindi hiki kigumu cha huzuni na majonzi ya kuondokewa na vijana wetu shupavu.
“Namuomba Mwenyezi Mungu atupe moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Dkt. Magufuli amelaani tukio hilo na matukio yote ya kuwashambulia askari polisi ambao wanafanya kazi kubwa na muhimu ya kulinda raia na mali na ametaka Watanzania wote watoe ushirikiano katika kukomesha vitendo hivyo. Mhe. Rais Magufuli amewaombea marehemu wote wapumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Askari hao walishambuliwa kwa risasi na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi walipokuwa wakitoka kubadilishana lindo. Wakiwa ndani ya gari ya polisi wakishuka katika mteremko walianza kushambulia gari mbele ambapo dreva alipoteza uelekeona kuingia mtaroni na kuendelea kuwashambulia kabla ya kufanikiwa kupora baadhi ya silaha walizokuwa nazo.