Jeshi la Polisi kuingiza sera ya UKIMWI katika mitaala wa kufundishia

 

KATIKA kuendeleza jitihada za kupunguza maambukizi ya VVU nchini, Jeshi la Polisi linakusudia kuingiza sera ya UKIMWI sehemu za kazi katika mitaala yao ya kufundishi katika vyuo vya mafunzo ya awali ya Jeshi hilo.

Lengo la kuingiza mitaala hiyo katika mafunzo ya awali ni utekelezaji wa mambo mbalimbali yaliyoandaliwa na Jeshi hilo katika awamu ya nne ili kutoa fursa kwa askari polisi wanaojiunga na fani hiyo na waliopo kazini
katika ngazi zote kuijua sera hiyo na kuitekeleza katika majukumu
yao ya kazi na familia zao.

Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Mafunzo wa Jeshi la Polisi ACP Bwelela Kilonzo wakati akifungua mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu sera ya UKIMWI katika Mradi wa afya unaotekelezwa na “Taasisi ya Marie Stopes” na kuratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za UKIMWI Tanzania (AJAAT).

Bwana Kilonzo alisema kuwa, mbali na mafunzo hayo kutolewa kwa askari wapya, pia askari walio kazini watapata nafasi ya kuijua sera hiyo kupitia mpango wa mafunzo kazini na semina mbalimbali za watendaji wa ngazi za juu zinazotolewa na Jeshi hilo katika mikakati yake ya kuboresha utendaji wa jeshi.
“Mwaka 2005 serikali ya awamu ya nne ilikuwa katika mpango wa maboresho mbalimbali pamoja na kutoa mafunzo kwa watumishi kutokana na utafiti uliofanywa ambapo waliangalia mapungufu na kubaini kuwepo katika masuala ya haki za binadamu, jinsia na UKIMWI na mwaka 2006 maeneo hayo yakapewa kipaumbele na kuwekewa msisitizo katika semina, hotuba na mikutano mbalimbali.

“Pamoja na kupewa kipaumbele pia walibaini kuwa suala la UKIMWI linapaswa kuingizwa katika mitaala ambapo waliamua kuibua hoja ya kutunga sera ya UKIMWI mahali pa kazi ili kuongeza nguvu katika utekelezaji na sera hiyo inatarajia kuingizwa rasmi katika mitaala Oktoba mwaka huu baada ya sera hiyo kuzinduliwa rasmi ,” alisema Bwana Kilonzo.
Alisema kuwa mikakati inayoendelea sasa ni kuhakikisha kuwa wanapitia maeneo mbalimbali ili kuweka mtiririko mzuri katika ufundishaji ili kuleta tija katika Jeshi hilo, familia, na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia kuhusu suala la mwamko wa upimaji wa hiari katika Jeshi hilo na familia zao, Kamanda wa Kikosi cha Polisi Tanzania, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi Nchini, ACP Serecky Msuya alisema kuwa ni mkubwa ambapo maambukizi ya VVU yamepungua kutoka asilimia 9 mwaka 2001/2008 hadi kufikia asilimia 5.7 sasa hivi.
Akizungumzia kuhusu kampeni ya utekelezaji wa mradi wa sera ya UKIMWI katika mikoa mingine, ACP Msuya alisema kuwa itategemea na mafanikio ya mikoa mitatu ya Dar es Salaam, Mbeya na Iringa ambapo mradi huu umeanza kutekelezwa kwa majaribio.

Chanzo: AJAAT, Joyce Magoti