NMB Yafadhili Mkutano wa Maofisa Waandamizi Dodoma

Kaimu Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa NMB, Bw. Abdulmajid Nsekela (kulia) akikabidhi mfano wa hundi ya shilingi Milioni 50 kwa Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini, Mh. Mwigulu Nchemba (katikati) kama udhamini wa mkutano mkuu wa mwaka wa Maofisa waandamizi wa Polisi na Makamanda wa Mikoa nchini. Mfano wa hundi hiyo imekabidhiwa mara baada ya ufunguzi wa mkutano unaoendelea mjini Dodoma. Kushoto ni Inspecta Jenerali wa Polisi nchini, IGP Ernest Mangu.

 

Mgeni Rasmi wa Mkutano Mkuu wa Jeshi la Polisi unaoendelea mkoani Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini, Mh. Mwigulu Nchemba (katikati) pamoja na Kaimu Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na wa Kati wa NMB, Bw. Abdulmajid Nsekela ( wa kwanza kulia) na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Ernest Mangu (wa kwanza kushoto) wakionesha mfano wa hundi ya shilingi Milioni 50 iliyotolewa na Benki ya NMB kwa ajili ya mkutano huo.

 

BENKI ya NMB imekabidhi udhamini wa shilingi Milioni 50 kwa jeshi la polisi kwaajili ya kufanikisha mkutano mkuu wa jeshi la polisi unaoendelea mkoani Dodoma kwa siku tatu. Mkutano huo unajumuisha maafisa waandamizi wa polisi na makamanda wa mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.

Udhamini huu unalenga kufanikisha mkutano huo wenye malengo ya kujadiri changamoto na mafanikio yaliyopatikana na jeshi la polisi kwa mwaka 2016 na kuweka mipango bayana ya usalama kwa mwaka 2017.

Akikabidhi hundi ya mfano kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi – Mh Mwigulu Nchemba, Kaimu Afisa Mkuu wa wateja Wadogo na wa Kati wa NMB – Abdulmajid Nsekela alisema kuwa udhamini huo unalenga kutambua umuhimu wa jeshi la polisi si tu kwa NMB bali kwa jamii yote kwa ujumla huku akisisitiza kuwa utendaji kazi mzuri wa jeshi la polisi umekuwa chachu ya maendeleo ya sekta ya kibenki nchini kwani benki zimekuwa zikifanya kazi katika mazingira tulivu bila matukio mengi ya uhalifu.

“Niseme tu kuwa jeshi la polisi wamekuwa wadau wetu wakubwa katika nyanja za ulinzi na pia biashara na hivyo hatuwezi kusita kudhamini mkutano huu mkubwa na muhimu kwa nchi yetu, tumekuwa tukitoa mchango kwa miaka kadhaa sasa kwa mkutano mkuu wa jeshi la polisi, na awamu hii, tumetoa mchango wa shilingi Milioni 50 ili kufanikisha mkutano,” alisema Bwana Nsekela.

Ndugu Nsekela pia alilishukuru jeshi la polisi kwa kutambua mchango wa NMB na kuwapatia Nafasi ya kufanya kazi pamoja. NMB pia ilitoa wasilisho la huduma mbalimbali ambazo imekuwa ikitoa kwa jeshi la polisi.

 

Kaimu Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na Kati, Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa wasilisho la huduma za kibenki kwa jeshi la polisi (hawapo Pichani) kwenye mkutano mkuu wa jeshi la polisi mkoani Dodoma.

 

Mgeni Rasmi wa Mkutano Mkuu wa Jeshi la Polisi unaoendelea mkoani Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani Nchini, Mh. Mwigulu Nchemba pamoja na Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, Ernest Mangu, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma – Jordan Rugimbana pamoja na Naibu Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Abdulrahman Kaniki wakiwa wanatoa heshima kwa wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini kabla ya ufunguzi rasmi.

 

Katika wasilisho hilo, NMB iliainisha mafanikio mbalimbali ambayo imeyafikia katika utoaji huduma na kuingizia serikali mapato huku ikielezwa kuwa tangu mwaka 2010, NMB imelipa kwa serikali jumla ya shilingi bilioni 336 kama kodi huku serikali ikinufaika na jumla ya shilingi bilioni 50 kama gawio kutoka NMB tangu mwaka 2010, NMB pia imelipa gawio la zaidi ya shilingi bilioni 174 tangu mwaka 2010. Thamani ya hisa serikali zilizoko NMB yaani asilimia 31.8 ni shilingi bilioni 437.

Ndugu Abdulmajid aliongeza kuwa “Tumekuwa tukifanya kazi vizuri na jeshi la polisi kwani kwa upande wa mikopo tu, mpaka sasa, mikopo yenye thamani ya shilingi Bilioni 27 imetolewa kwa zaidi ya askari polisi 8,569 kupitia mikopo ya mishahara.”
NMB ndiyo benki inayoongoza nchini kwa kuwa na matawi mengi kwani ina matawi zaidi ya 189 yaliyopo karibia kila wilaya, ATM Zaidi ya 700 nchi nzima pamoja na idadi ya wateja inayofikia milioni mbili na nusu.