RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 23 Machi, 2017 amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri. Katika Mabadiliko hayo, Mhe. Rais Magufuli amemteua Prof. Palamagamba Mwaluko Kabudi kuwa Waziri wa Katiba na Sheria na hapo hapo Dkt. Magufuli amemteua Dkt. Harrison George Mwakyembe kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo nafasi ambayo awali ilikuwa ikishikwa na Nape Nnauye (pichani). Katika taarifa hiyo ya ikulu iliyotolewa leo inaeleza uteuzi huu unaanza mara moja.
Taarifa hiyo ya Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU, Gerson Msigwa imefafanua kuwa wateule wote wataapishwa kesho Mchana tarehe 24 Machi, 2017 Ikulu, Jijini Dar es Salaam. Hata hivyo haikufafanua chochote kuhusu aliyekuwa Waziri katika nafasi hiyo, Nape Nnauye anakwenda kushika nafasi gani kwa sasa.
Awali kufuatia tuhuma za uvamizi wa kituo cha Clouds FM hivi karibuni zinazodaiwa kufanywa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Mnauye aliunda kamati ambayo ilitoka na taarifa iliyosomwa jana katika vyombo vya habari.
Wachambuzi wa masuala ya siasa wanahusisha mabadiliko hayo ni kwa kitendo cha Nape kuunda Kamati kuchunguza tukio la tuhuma za uvamizi wa Paul Makonda unaodaiwa kufanywa katika kituo cha Clouds FM.