Waziri Muhongo Azinduwa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini, Pwani

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye fulana ya Bluu) na Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakifukia nguzo ya umeme kwa udongo ikiwa ni ishara ya kuanza kwa utekelezaji wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu katika mkoa wa Pwani.

 




 Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye fulana ya Bluu) na Mbunge wa Chalinze, Mhe. Ridhiwani Kikwete wakifungua kitambaa kuashiria uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini, Awamu ya Tatu katika mkoa wa Pwani.
Watendaji kutoka kampuni ya Steg International Services wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini (hayupo pichani) wakati wa Uzinduzi wa Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini Awamu ya Tatu katika mkoa wa Pwani. Kampuni hiyo itatekeleza sehemu ya kwanza ya Mradi huo wa Awamu ya Tatu.
Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
WAZIRI wa Nishati na Madini, prof. Sospeter Muhongo amezindua mradi wa umeme vijijini (REA) awamu ya tatu katika Mkoa wa Pwani na kudai mkoa huo utapewa kipaombele kwani ni kimbilio la wawekezaji na ukanda wa viwanda.
Aidha amewataka watanzania kuacha kujidharau kupitia mradi huo kutokana ni mkombozi wa wananchi .
Mbali ya hayo, Pro. Muhongo anasema, mwaka 2007 kulikuwa na asilimia 2 pekee ya watumiaji wa nishati ya umeme lakini kwa sasa kasi inakua ambapo imefikia asilimia 49.5.
Akizindua awamu ya tatu ya mradi huo na kumtambulisha mkandarasi kutoka Tunisia kampuni ya Steg katika mkoa huo,alisema ni wakati wa kuchangamkia fursa hiyo kwa kila mtanzania mwenye mahitaji ya umeme.
Alisema katika awamu hiyo, imetengwa kiasi cha sh. trilioni moja ambapo vijiji 3,559 vitafikiwa nchini na mkoa wa Pwani vitafikiwa vijiji 150 vilivyokuwa havijafikiwa kwenye awamu ya kwanza na ya pili.
“Malengo yetu ni kuvifikia vijiji vyote 12,268 nchini, kwa kutumia umeme kupitia Tanesco na mradi huu wa umeme vijijini ili kila mmoja anufaike nao na kuondokana na kutumia vibatari,” alisema.
Hata hivyo, Pro. Muhongo alisema, wakati mradi wa REA awamu ya tatu ukianza katika maeneo mbalimbali nchini ni lazima upelekwe katika taasisi ikiwemo zahanati,shule na madhehebu ya dini .
Alisema mkoa wa Pwani ni mkoa kati ya mikoa iliyojikita katika viwanda na uwekezaji hivyo ni lazima nguvu kubwa ielekezwe huko.
Pro. Muhongo alimtaka mkuu wa mkoa wa Pwani kuwaweka tayari wataalamu wake wa mkoa, na wataalamu wa Tanesco , REA, wabunge na meneja wa kanda ,ili kuweza kubainisha mahitaji yote ambayo yatarahisisha kufanyiwa kazi na wizara.
Aliwaomba wananchi watakaopitiwa na miundombinu ya umeme vijijini kutotaka fidia ili serikali iweze kufanikisha malengo yake na kuinua maendeleo ya watanzania.

Pro.Muhongo alisema kuwa fedha zilizotengwa ambazo ni karibu trilioni moja zilizotengwa kwa ajili ya mradi huo hazitakuwa sehemu ya fidia kwa ajili ya maeneo umeme huo utakapopita.
“Bajeti iliyopangwa kutumika kwenye awamu hii kwa nchi nzima ni mara tatu ya bajeti iliyopita 
huku fedha hizo zikiwa ni za ndani hivyo wananchi wajitolee pasipo kudai fidia,” alisema.
Waziri huyo,alieleza kwamba, serikali imedhamiria kufikisha umeme kwa watanzania , kwa malipo yenye gharama nafuu ya.sh.27.000 sawa na majogoo mawili.
Prof. Muhongo, alimpongeza mkuu wa mkoa wa Pwani, kwa kukuza sekta ya viwanda na uwekezaji, pamoja na mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete na wa Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa kwa kupigania maendeleo ya majimbo yao.
Nae mkurugenzi wa REA Injinia, Gisima Nyamo-Hanga alisema ,moja ya changamoto zinazowakabili ni baadhi ya wananchi kudai fidia kwa maeneo ambayo miundombinu ya umeme inapopitishwa.
Mkuu wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo alisema kuwa mkoa huo unakabiliwa na changamoto ya wateja kuhitaji kuunganishiwa umeme lakini vifaa kama vile nguzo, mita na nyaya ni vichache.
Ndikilo aliomba mkoa huo uongezewe nguvu ya umeme megawatt  60 ambapo kwasasa wanapata megawati 38 hadi 40 ambazo hazikidhi mahitaji ukizingatia mkoa umesheheni viwanda.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chalinze Ridhiwani Kikwete alieleza mahitaji ya umeme ni makubwa katika vijiji vilivyopo Chalinze .


Aliomba mahitaji mapya yaingizwe kwenye bajeti kwa lengo la kufanyiwa kazi katika bajeti ya 2017-2018.

Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini Hamoud Jumaa alisema kuwa baadhi ya vijiji kama Gwata, Lukenge, Mpiji na baadhi ya misikiti, shule na zahanati havina umeme hivyo kushindwa kujiendeleza.