Prof Waziri Mbarawa Uso kwa Uso na Bodi ya AfDB

Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa (wa kwanza kushoto ), akifafanua jambo kwa wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo Africa (AfDB), bi, Lekhethe Mmakgoshi, Dkt. Weggoro Nyamajeje na Dkt. Bright Okogu (wa kwanza kulia), alipokutana na Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo kujadiliana namna ya kushirikiana kuboresha sekta ya miundombinu ya uchukuzi hapa nchini.

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameiomba Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya Maendeleo Africa (AfDB), kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika mkakati wake wa kukuza uchumi kwa kuwekeza katika sekta ya miundombinu.
Akizungumza na Wakurugenzi wa Bodi ya AfDB waliomtembelea ofisini kwake jijini Dar es Salaam leo Prof. Mbarawa ameishukuru benki hiyo kwa ushirikiano inaoipa Serikali ya Tanzania katika miradi mingi ya ujenzi wa barabara na kuiomba kuiunga mkono katika uwekezaji mkubwa inaoufanya katika miradi ya usafiri wa anga na reli.
“Tumejipanga kukuza uchumi kwa kuimarisha sekta za barabara,anga,reli na bandari hivyo tunaomba ushirikiano wenu kadri tunavyouhitaji ili kufikia malengo yetu kwa wakati”, amesema Prof. Mbarawa.
Ameitaja baadhi ya miradi ya barabara ambayo Tanzania imenufaika na AfDB kuwa ni barabara ya Kibondo-Kasulu-Manyovu Km 250, Makutano-Nata-Mugumu-Mto wa Mbu hadi Loliondo Km 213, Makurunge-Saadani-Pangani-Tanga KM 178 na barabara za pete jijini Dar es Salaam Km 34.
“Kuimarika kwa Sekta ya miundombinu nchini hasa sekta ya anga, reli na barabara, kutaimarisha sekta za utalii na kilimo na hivyo kuongeza ajira na kukuza uchumi wa taifa”, amesisitiza Prof. Mbarawa.
Naye mjumbe wa Bodi ya AfDB Dkt. Weggoro Nyamajeje Calleb amezungumzia umuhimu wa miradi ya ujenzi inayoanzishwa hapa nchini kutoa fursa za ajira kwa wananchi na kuwekewa mazingira endelevu ili ilete mabadiliko chanya katika maisha ya watu na taifa kwa ujumla.
Dkt. Calleb amesisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika ujenzi wa miundombinu ili kuiwezesha nchi kuwa na miundombinu bora na yakutosha na hivyo kuchochea maendeleo.
Ujumbe wa AfDB upo hapa nchini ambapo pamoja na mambo mengine leo umepata fursa ya kubadilishana uzoefu na viongozi wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano ili kujua mikakati yake katika kuboresha miundombinu hapa nchini na namna inavyoweza kutoa ushirikiano katika kuiwezesha.

Imetolewa na Kitengo cha Habari na Mawasiliano Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.