SERIKALI imesema itatuma wataalam wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Nchini (TAA), kuangalia Maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya Ujenzi wa Viwanja vya ndege katika Wilaya ya Masasi na Tunduru ili kujiridhisha na kushauri Serikali namna ya kutekeleza miradi hiyo.
Akizungumza mara baada ya kuonyeshwa maeneo hayo Waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa amesema pamoja na maeneo hayo kutengwa na Wilaya hizo kuna ulazima wa kuwatuma wataalam wa Viwanja ili kuwa na Viwanja bora vinavyozingatia viwango vya kimataifa.
“Nawapongeza sana kwa kutenga maeneo kwa ajili ya kujengaViwanja vya ndege kwani ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi, hivyo ili kukidhi viwango vilivyowekwa kimataifa katika ujenzi wa viwanja vya ndege nitatuma wataalam kutoka TAA ili kukagua maeneo haya na watoe muelekeo kwa kuishauri Serikali kuhusu utekelezaji wa miradi hii muhimu”, amesisitiza Waziri Prof. Mbarawa.
Kuhusu kiwanja cha Masasi Waziri Mbarawa ameiagiza TAA na Halmashauri ya Wilaya yaMasasi kukaa pamoja na kuainisha mipaka ya kiwanja hicho ili kuepuka uvamizi wa miundombinu ya kiwanja hicho.
Aidha, Waziri Prof. Mbarawa amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo kuiandikia Wizara mahitaji ya eneo hilo na kuainisha sababu ya kuhamisha kiwanja cha ndege cha Tunduru kutoka mjini kwenda nje ya mji.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), mkoani Mtwara, Bi. Zitta Majinge, amemhakikishia Waziri huyo kuleta maombi ya mapendekezo ya viwanja hivyo makao makuu ili kuweza kutafutiwa ufumbuzi wa changamoto za viwanja hivyo.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.