RC Morogoro awaasa waandishi wa michezo

Mmoja wa waandishi wa habari wa michezo akijibu swali aliloulizwa na Mwalimu wa waandishi wa habari ambae ni mkufunzi Said Salim, katika semina ya kuwanoa waandishi wa habari za michezo wanaoshiriki semina hiyo iliyoandaliwa na Taswa na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania, Mjini Morogoro.

Na Mwandishi Wetu, Morogoro

MKUU wa Mkoa wa Morogoro, Joel Bendera amewataka waandishi wa habari za michezo kuacha dhana potofu ya kuripoti habari za uchochezi na badala yake waripoti habari zinazoelimisha jamii kwa ujumla.

Bendera ametoa kauli hiyo leo wakati wa semina ya waandishi wa habari za michezo waliohudhuria mafunzo yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo nchini (TASWA) yaliyofanyika mkoani Morogoro.

Mkuu huyo alisema kumekuwa na mtindo wa waandishi wengi kupenda kuripoti habari za migogoro jambo ambalo linachochea migogoro na kusababisha kushusha taaluma ya michezo nchini.

Changamoto kama hiyo pia imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Halima Dendego ambaye alifunga mafunzo hayo yaliyoshirikisha jumla ya waandishi 40 kutoka mikoa ya Pwani, Morogoro na Dar es Salaam, chini ya udhamini wa kampuni ya mawasiliano Vodacom Tanzania.

Akizungumza na waandishi wakati akifunga mafunzo hayo alisema waandishi wa michezo wanatakiwa kuacha ushabiki wa Simba na Yanga kitendo ambacho kinachangia kupotosha sekta nzima ya uandishi wa habari za michezo. “Nawaomba mzingatie mafunzo mliopata ili kuboresha zaidi sekta ya habari za michezo,” alisema Dendego.

Alisema TASWA imefanya jambo la msingi kuandaa mafunzo hayo kitendo ambacho kimetoa changamoto kwa wanahabari kuripoti habari znye usahihi tofauti na vyo saa wmekuwa wakiripoti habari za ushabkzaidi

Baadhi ya waandishi wa habari za michezo wakiwa katika semina ya kuwanoa waandishi wa habari za michezo iliyoandaliwa na Taswa na kudhaminiwa na Vodacom Tanzania, Mjini Morogoro.


Aliongeza kusema si kila siku mnaegemea kuandika migogoro na habari ambazo hazina tija kwa jamii ya wanamichezo wa Tanzania mnatakiwa kuandika habari ya uhakika kutokana na kwamba waandishi ni kioo cha jamii.

Alisema kutokana na mafunzo hayo, waandishi hao watakuwa wamekwiva vya kutosha na matunda yake anayategemea kuyaona watakavyorejea katika vyombo vyao vya habari.

Aliwashukuru wadhamini wa mafunzo hayo, Kampuni ya Simu za Mkononi Vodacom na wadhamini washiriki kampuni ya mabasi ya Al Saedy Bus Service kwa kujitolea kudhamini mafunzo hayo.

Hata hivyo ameahidi kushirikiana na TASWA bega kwa bega katika kuendeleza michezo nchini, kwa sababu kuna mingine kama mpira wa wavu na netiboli imedorora.

Kwa upande wa Vodacom kupitia Meneja Uhusiano na Habari za Mtandao, Matina Nkurlu alisema, kutokana na kampuni hiyo, kwa muda mrefu imekuwa mdau muhimu katika kuendeleza sekta ya michezo Kitaifa na Kimataifa nchini haikusita kudhamini mafunzo hayo.

“Vodacom imekuwa ikidhamini michezo mbalimbali, kama Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, Vodacom Miss Tanzania, Mwanza Cycle Challenge, Kilimanjaro Marathon na Mashindano ya mbio za mashua za Vodacom Regata, imekuwa ikidhamini pia mafunzo ya kunoa waandishi wa habari kama ilivyofanya, alisema Matina.

Aliongeza kuwa: “Pamoja na kufanya biashara bado tunaona ni muhimu kutoa mchango katika hii ili kuiwezesha Tanzania siku moja kuwa moja ya nchi zinazofanya vizuri kwenye michezo kama tunavyosikia majina ya nchji za Nigeria, Ghana, Afrika Kusini na nyingine.’’